Mhubiri - Sura ya 3

Mhubiri - Sura ya 3

1Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.

2Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa;

3Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga;

4Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza;

5Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia;

6Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa;

7Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena;

8Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.

9Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo?

10Nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake.

11Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.

12Mimi najua ya kwamba hakuna jema kwao kupita kufurahi, na kufanya mema maadamu wanaishi.

13Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote.

14Najua ya kwamba kila kazi aifanyayo Mungu itadumu milele; haiwezekani kuizidisha kitu, wala kuipunguza kitu; nayo Mungu ameifanya ili watu wamche Yeye.

15Yale yaliyoko yamekuwako; na hayo yatakayokuwako yamekwisha kuwako; naye Mungu huyatafuta tena mambo yale yaliyopita.

16Zaidi ya hayo, nikaona tena chini ya jua ya kwamba, Mahali pa hukumu upo uovu, Na mahali pa haki upo udhalimu.

17Nikasema moyoni mwangu, Mungu atawahukumu wenye haki na wasio haki; kwa kuwa kuna wakati huko kwa kila kusudi na kwa kila kazi.

18Nikasema moyoni mwangu, Ni kwa sababu ya wanadamu, ili Mungu awajaribu, nao waone ya kuwa wao wenyewe wafanana na wanyama.

19Kwa maana linalowatukia wanadamu linawatukia wanyama; jambo moja lawatukia; anavyokufa huyu ndivyo anavyokufa huyu; naam, wote wanayo pumzi moja; wala mwanadamu hana kitu cha kumpita mnyama; kwa maana yote ni ubatili.

20Wote huendea mahali pamoja; wote hutoka katika mavumbi; na hata mavumbini hurudi tena.

21Ni nani ajuaye kama roho ya binadamu huenda juu, na kama roho ya mnyama huenda chini?

22Hivyo nikaona ya kwamba hakuna jema kupita mwanadamu kuzifurahia kazi zake; kwa sababu hili ni fungu lake; kwa maana ni nani atakayemrudisha tena ili ayaone yatakayomfuata baadaye.