Mhubiri - Sura ya 6

Mhubiri - Sura ya 6

1Kuna baa nililoliona mimi chini ya jua, nalo linawalemea wanadamu kwa uzito;

2mtu aliyepewa na Mungu mali, ukwasi, na heshima, hata asipungukiwe na kitu cho chote kwa nafsi yake, katika yote anayoyatamani walakini Mungu hamwezeshi kula katika hizo; bali mgeni hula. Hayo ndiyo ubatili hasa, nayo ni ugonjwa mbaya.

3Mtu akizaa watoto mia, akaishi miaka mingi, nazo siku za maisha yake ni nyingi, lakini nafsi yake haikushiba mema; tena ikiwa, zaidi ya hayo, amekosa maziko; mimi nasema, Heri mimba iliyoharibika kuliko huyo;

4yaani, hiyo huja katika ubatili, na huenda gizani, nalo jina lake limefunikwa giza;

5tena, haikuliona jua wala kulifahamu; basi, hii imepata kustarehe kuliko yule;

6naam, ajapoishi miaka elfu mara mbili, asijiburudishe kwa mema; je! Wote hawaendi mahali pamoja?

7Kazi yote ya binadamu ni kwa kinywa chake, Walakini hata hivyo nafsi yake hashibi.

8Kwa maana mwenye hekima hupata faida gani kuliko mpumbavu? Au maskini ana nini kuliko yeye ajuaye kwenda mbele ya walio hai?

9Heri kuona kwa macho, Kuliko kutanga-tanga kwa tamaa.

10Na awe kitu cho chote, aliitwa jina lake zamani za kale, naye amejulikana kuwa ndiye mwanadamu; wala hawezi kabisa kushindana na yeye aliye na uwezo kuliko yeye mwenyewe.

11Basi, kwa kuwa kuna mambo mengi yaongezayo ubatili, mwanadamu hufaidiwa nini?

12Kwa maana ni nani ajuaye yaliyo mema ya mwanadamu katika maisha yake, siku zote za maisha yake ya ubatili, anayoishi kama kivuli? Kwa maana ni nani awezaye kumweleza mwanadamu mambo yatakayofuata baada yake chini ya jua?