Mhubiri - Sura ya 9

Mhubiri - Sura ya 9

1Na kwa ajili ya hayo yote, nikatia moyo wangu katika kuyatafuta-tafuta haya; ya kuwa wenye haki, na wenye hekima, pamoja na matendo yao yote, wamo mkononi mwa Mungu; kwamba ni pendo au kwamba ni chuki, mwanadamu hajui; mambo yote yawapita.

2Mambo yote yawatukia wote sawasawa; kuna tukio moja kwake mwenye haki na kwake asiye haki; kwa mtu mwema na kwa mtu mwovu; kwa mtu aliye safi na kwa mtu asiye safi; kwake yeye atoaye kafara na kwake asiyetoa kafara; kama alivyo huyo mwema ndivyo alivyo mwenye dhambi; yeye aapaye na yeye aogopaye kiapo.

3Baa hilo ni katika mambo yote yanayofanyika chini ya jua, ya kuwa wote wanalo tukio moja; naam, zaidi ya hayo, mioyo ya wanadamu imejaa maovu, na wazimu umo mioyoni mwao wakati walipo hai, na baadaye huenda kwa wafu.

4Kwa kuwa liko tumaini kwa yule aliyeambatana na wote walio hai; (maana ni afadhali mbwa aliye hai kuliko simba aliyekufa);

5kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa.

6Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote lililofanyika chini ya jua.

7Wewe enenda zako, ule chakula chako kwa furaha, unywe mvinyo yako kwa moyo wa kuchangamka; kwa kuwa Mungu amekwisha kuzikubali kazi zako.

8Mavazi yako na yawe meupe sikuzote; wala kichwa chako kisikose marhamu.

9Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili, ulizopewa chini ya jua; siku zote za ubatili wako, kwa maana huo ni sehemu yako ya maisha; na katika taabu zako ulizozitaabika chini ya jua.

10Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe.

11Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote.

12Maana mwanadamu naye hajui wakati wake; kama samaki wanaokamatwa katika nyavu mbaya, na mfano wa ndege wanaonaswa mtegoni, kadhalika wanadamu hunaswa katika wakati mbaya, unapowaangukia kwa ghafula.

13Pia nimeona hekima chini ya jua, nayo ni kama hivi, tena kwangu mimi ilionekana kuwa ni neno kubwa.

14Palikuwa na mji mdogo, na watu ndani yake walikuwa wachache; akaja mfalme mkuu juu yake, akauhusuru, akajenga ngome kubwa ili kuupiga.

15Basi, kulionekana humo mtu maskini mwenye hekima, naye kwa hekima yake akauokoa mji ule lakini hata hivyo hapakuwa na mtu ye yote aliyemkumbuka yule mtu maskini.

16Ndipo niliposema, Bora hekima kuliko nguvu; walakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi.

17Maneno ya wenye hekima yanenwayo taratibu husikiwa, Zaidi ya mlio wake atawalaye katikati ya wapumbavu.

18Hekima ndiyo bora kupita silaha za vita; Lakini mkosaji mmoja huharibu mema mengi.