Waefeso - Sura ya 3

Waefeso - Sura ya 3

1Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa;

2ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu;

3ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache.

4Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo.

5Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;

6ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili;

7Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake.

8Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika;

9na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote;

10ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho;

11kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu.

12Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.

13Basi naomba msikate tamaa kwa sababu ya dhiki zangu kwa ajili yenu, zilizo utukufu kwenu.

14Kwa hiyo nampigia Baba magoti,

15ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa,

16awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani.

17Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo;

18ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina;

19na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.

20Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;

21naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.