Waefeso - Sura ya 4

Waefeso - Sura ya 4

1Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa;

2kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo;

3na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

4Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.

5Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.

6Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.

7Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo.

8Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa.

9Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi?

10Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote.

11Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;

12kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;

13hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;

14ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.

15Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.

16Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.

17Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao;

18ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao;

19ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani.

20Bali ninyi, sivyo mlivyojifunza Kristo;

21ikiwa mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika Yesu,

22mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya;

23na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu;

24mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.

25Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.

26Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;

27wala msimpe Ibilisi nafasi.

28Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji.

29Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.

30Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.

31Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;

32tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.