Waefeso - Sura ya 5

1Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa;
2mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.
3Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;
4wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru.
5Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu.
6Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi.
7Basi msishirikiane nao.
8Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru,
9kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli;
10mkihakiki ni nini impendezayo Bwana.
11Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee;
12kwa kuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena.
13Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru.
14Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.
15Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima;
16mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.
17Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.
18Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;
19mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu;
20na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo;
21hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo.
22Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu.
23Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.
24Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.
25Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;
26ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;
27apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.
28Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.
29Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.
30Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake.
31Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.
32Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa.
33Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.