Waefeso - Sura ya 6

Waefeso - Sura ya 6

1Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.

2Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,

3Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.

4Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.

5Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni kumtii Kristo;

6wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekazao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo;

7kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu;

8mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana kwamba ni mtumwa au kwamba ni huru.

9Nanyi, akina bwana, watendeeni wao yayo hayo, mkiacha kuwaogofya, huku mkijua ya kuwa yeye aliye Bwana wao na wenu yuko mbinguni, wala kwake hakuna upendeleo.

10Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.

11Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

16zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;

18kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

19pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili;

20ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena.

21Basi ninyi nanyi mpate kuzijua habari zangu, ni hali gani, Tikiko, ndugu mpendwa, mhudumu mwaminifu katika Bwana, atawajulisheni mambo yote;

22ambaye nampeleka kwenu kwa kusudi lilo hilo mpate kuzijua habari zetu, naye awafariji mioyo yenu.

23Amani na iwe kwa ndugu, na pendo, pamoja na imani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo.

24Neema na iwe pamoja na wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo katika hali ya kutokuharibika.