Esta - Sura ya 4

Esta - Sura ya 4

1Basi Mordeikai alipojua mambo yote yaliyofanyika, alizirarua nguo zake, akajivika gunia pamoja na majivu, akatoka hata kufika katikati ya mji, akalia kwa sauti kuu ya uchungu.

2Pia akafika hata mbele ya mlango wa mfalme; maana hakuna awezaye kuingia ndani ya mlango wa mfalme hali amevaa magunia.

3Na katika kila jimbo, ambako amri ya mfalme na mbiu yake imewasili, palikuwako msiba mkuu kwa Wayahudi, na kufunga, na kulia, na kuomboleza; hata na wengi wakalala juu ya gunia na majivu.

4Basi wajakazi wake Esta, na wasimamizi wake wa nyumba, wakamjia, wakampasha habari; naye malkia akahuzunika mno; akampelekea Mordekai mavazi, ili kumvika, na kumwondolea gunia lake; walakini yeye asikubali.

5Kisha Esta akamwita Hathaki, msimamizi-wa-nyumba mmojawapo wa mfalme, aliyemwagiza amhudumu Esta, akamtuma kwa Mordekai, ili ajue mambo hayo, na maana yake ni nini.

6Basi yule Hathaki akatoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanda wa mji ulipo mbele ya mlango wa mfalme.

7Naye Mordekai akamweleza yote yaliyompata, na hesabu ya fedha Hamani aliyoahidi kulipa katika hazina ya mfalme, ili Wayahudi waangamizwe.

8Pia akampa na nakili ya andiko la mbiu ya kuwaangamiza, iliyotangazwa Shushani, ili amwonyeshe Esta, na kumweleza; tena amwagize aingie kwa mfalme, kumsihi na kuwaombea watu wake.

9Basi Hathaki akaja, akamwambia Esta maneno ya Mordekai.

10Ndipo Esta akasema na Hathaki, akamtuma tena kwa Mordekai, kusema,

11Watumwa wote wa mfalme wanajua sana, hata na watu wa majimbo ya mfalme, ya kwamba mtu ye yote, akiwa mwanamume au mwanamke, atakayemjia mfalme katika ua wa ndani, wala hakuitwa, kuna sheria moja kwake, ni kwamba auawe; isipokuwa yeye ambaye mfalme atamnyoshea fimbo ya dhahabu, ili aishi; wala mimi sikuitwa niingie kwa mfalme yapata siku thelathini.

12Basi wakamwambia Mordekai maneno ya Esta.

13Naye Mordekai akawaagiza wampelekee Esta jibu la kusema, Wewe usijidhanie kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote.

14Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?

15Basi Esta akawatuma ili wamjibu Mordekai,

16Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.

17Basi Mordekai akaenda zake, akafanya yote kama vile Esta alivyomwagiza.