Esta - Sura ya 6

Esta - Sura ya 6

1Usiku ule mfalme hakupata usingizi; akaamuru aletewe kitabu cha maandiko ya taarifa, nayo yakasomwa mbele ya mfalme.

2Ikaonekana kuwa imeandikwa ya kwamba Mordekai aliwachongea Bigthana na Tereshi, wasimamizi wawili wa mfalme, katika hao waliolinda mlango, waliotaka kumtia mikono mfalme Ahasuero.

3Mfalme akasema, Je! Ni heshima gani au jaha gani Mordekai aliyofanyiziwa kwa ajili ya hayo? Watumwa wa mfalme waliomhudumu wakamwambia, Hakuna alilofanyiziwa.

4Mfalme akasema, Yupo nani behewani? Ikawa Hamani alikuwa ameingia katika ua wa nje wa nyumba ya mfalme, aseme na mfalme, ili kumtundika Mordekai juu ya mti ule aliomwekea tayari.

5Basi watumwa wa mfalme wakamwambia, Tazama, Hamani yupo, amesimama behewani. Mfalme akasema, Na aingie.

6Basi Hamani akaingia. Mfalme akamwambia, Afanyiziwe nini yule ambaye mfalme apenda kumheshimu? Hamani akasema moyoni mwake, Ni nani ambaye mfalme apenda kumheshimu kuliko mimi?

7Basi Hamani akamwambia mfalme, Yule ambaye mfalme apenda kumheshimu,

8na aletewe mavazi ya kifalme ambayo mfalme amezoea kuyavaa, na farasi ambaye mfalme humpanda mwenyewe, ambaye ametiwa taji ya kifalme kichwani;

9na yale mavazi na yule farasi akabidhiwe mkononi mmojawapo wa maakida wa mfalme aliye mstahiki; ili makusudi amvike yule ambaye mfalme apenda kumheshimu, na kumrakibisha juu ya farasi kuipitia njia kuu ya mjini, na kupiga mbiu mbele yake, kusema, Hivyo ndivyo atakavyofanyiziwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu.

10Basi mfalme akamwambia Hamani, Hima! Twaa mavazi na farasi kama ulivyosema, ukamfanyizie vivyo hivyo Mordekai, Myahudi, aketiye mlangoni pa mfalme; lisipungue neno lo lote katika yote uliyoyasema.

11Ndipo Hamani alipoyatwaa mavazi na farasi, akamvika Mordekai yale mavazi, akamrakibisha juu ya farasi kuipitia njia kuu ya mjini, akapiga mbiu mbele yake, Hivyo ndivyo atakavyofanyiziwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu.

12Kisha Mordekai akarudi kwenye mlango wa mfalme. Bali Hamani akaenda mbio nyumbani kwake, mwenye msiba, na kichwa chake kimefunikwa.

13Basi Hamani akawasimulia Zereshi mkewe na rafiki zake wote kila neno lililompata. Kisha watu wake wenye hekima na Zereshi mkewe wakamwambia, Ikiwa huyu Mordekai, ambaye umeanza kuanguka mbele yake, ni wa uzao wa Wayahudi, wewe hutamweza, bali kuanguka utaanguka mbele yake.

14Hata walipokuwa katika kusema naye, wasimamizi-wa-nyumba wa mfalme walifika, wakahimiza kumleta Hamani katika karamu ile aliyoiandaa Esta.