Kutoka - Sura ya 11

Kutoka - Sura ya 11

1Bwana akamwambia Musa, Liko pigo moja bado, nitakaloleta juu ya Farao na juu ya Misri; baadaye atawapa ninyi ruhusa mtoke huku; naye hapo atakapowapa ruhusa, atawafukuza mtoke huku kabisa kabisa.

2Basi nena wewe masikioni mwa watu hawa, na kila mtu mume na atake kwa jirani yake, na kila mwanamke atake kwa jirani yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu.

3Bwana akawapa watu hao kibali machoni pa Wamisri. Zaidi ya hayo, huyo Musa alikuwa ni mkuu sana katika nchi ya Misri, machoni pa watumishi wa Farao, na machoni pa watu wake.

4Musa akasema, Bwana asema hivi, Kama usiku wa manane mimi nitatoka nipite kati ya Misri;

5na wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri watakufa, tangu yule mzaliwa wa kwanza wa Farao aketiye katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa huyo kijakazi aliye pale nyuma ya jiwe la kusagia; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama.

6Ndipo kutakuwa na kilio kikuu katika nchi yote ya Misri, ambacho mfano wake haujakuwa bado majira yo yote, wala hautakuwako mfano wake tena kabisa.

7Lakini katika wana wa Israeli hapana hata mbwa atakayetoa ulimi juu yao, juu ya mtu wala juu ya mnyama; ili kwamba mpate kujua jinsi Bwana anavyowatenga Wamisri na Waisraeli.

8Tena hao watumishi wako wote watanitelemkia kwangu mimi, nao watanisujudia, wakisema, Toka wewe, na hawa watu wote wakufuatao; na baada ya hayo nitatoka. Basi akatoka kwa Farao na hasira kuu.

9Bwana akamwambia Musa, Farao hatawasikiza ninyi; kusudi ajabu zangu ziongezeke katika nchi ya Misri.

10Musa na Haruni walifanya ajabu hizo zote mbele ya Farao; Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake.