Kutoka - Sura ya 13

1Bwana akasema na Musa, akamwambia,
2Nitakasie mimi wazaliwa wa kwanza wote, kila afunguaye tumbo katika wana wa Israeli, wa binadamu na wa mnyama; ni wangu huyo.
3Musa akawaambia hao watu, Kumbukeni siku hii, mliyotoka nchi ya Misri, kutoka nyumba ya utumwa; kwa kuwa Bwana aliwatoa mahali hapa kwa nguvu za mkono wake; na usiliwe mkate uliochachwa.
4Ninyi mwatoka leo katika mwezi wa Abibu.
5Itakuwa hapo Bwana atakapowaleta mpaka nchi ya Wakanaani, na Wahiti, na Waamori, na Wahivi, na Wayebusi, nchi hiyo aliyowaapia baba zako kwamba atakupa wewe, ni nchi imiminikayo maziwa na asali, ndipo mtakapoushika utumishi huu katika mwezi huu.
6Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba, nayo siku ya saba itakuwa ni sikukuu ya Bwana.
7Mikate isiyochachwa italiwa katika hizo siku saba; mkate uliotiwa chachu usionekane kwako, wala chachu isionekane kwako, ndani ya mipaka yako yote.
8Nawe utamwambia mwanao siku hiyo, ukisema, Ni kwa sababu ya hayo Bwana aliyonifanyia hapo nilipotoka Misri.
9Nayo itakuwa ishara kwako katika mkono wako, na kwa ukumbusho kati ya macho yako, ili kwamba sheria ya Bwana ipate kuwa kinywani mwako; kwani Bwana alikutoa utoke Misri kwa mkono wenye uwezo.
10Kwa hiyo utaitunza amri hii kwa wakati wake mwaka baada ya mwaka.
11Itakuwa hapo Bwana atakapokuleta katika nchi ya Wakanaani, kama alivyokuapia wewe na baba zako, na kukupa,
12ndipo utamwekea Bwana kila afunguaye tumbo, na kila mzaliwa wa kwanza uliye naye, azaliwaye na mnyama; hao waume watakuwa ni wa Bwana.
13Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo; na kwamba hutaki kumkomboa, utamvunja shingo; na kila mzaliwa wa kwanza wa binadamu katika wanao utamkomboa.
14Kisha itakuwa hapo mwanao atakapokuuliza keshoni, akisema, Ni nini hivi? Utamwambia, Bwana alimtoa Misri, kutoka ile nyumba ya utumwa, kwa uwezo wa mkono wake;
15basi ilikuwa hapo Farao alipojifanya kuwa mgumu ili asitupe ruhusa kuondoka, Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote waliokuwa katika nchi ya Misri, wa binadamu na wa mnyama; kwa ajili ya hayo namtolea Bwana wote wafunguao tumbo, wakiwa waume; lakini wazaliwa wa kwanza wote wa wana wangu nawakomboa.
16Jambo hilo litakuwa ni ishara mkononi mwako, na utepe katikati ya macho yako; kwa kuwa Bwana alitutoa Misri kwa uwezo wa mkono wake.
17Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri;
18lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha.
19Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajilia ninyi; nanyi mtaichukua mfupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.
20Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa ile jangwa.
21Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku;
22ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.