Kutoka - Sura ya 15

Kutoka - Sura ya 15

1Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.

2Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.

3Bwana ni mtu wa vita, Bwana ndilo jina lake.

4Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu.

5Vilindi vimewafunikiza, Walizama vilindini kama jiwe.

6Bwana, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo, Bwana, mkono wako wa kuume wawaseta-seta adui.

7Kwa wingi wa ukuu wako wawaangusha chini wanaokuondokea, Wapeleka hasira yako, nayo huwateketeza kama mabua makavu.

8Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa, Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa chungu, Vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.

9Adui akasema, Nitafuatia, nitapata, nitagawanya nyara, Nafsi yangu itashibishwa na wao; Nitaufuta upanga wangu, mkono wangu utawaangamiza.

10Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza; Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu.

11Ee Bwana, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu?

12Ulinyosha mkono wako wa kuume, Nchi ikawameza.

13Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa, Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu.

14Kabila za watu wamesikia, wanatetemeka, Wakaao Ufilisti utungu umewashika.

15Ndipo majumbe wa Edomu wakashangaa, Watu wa Moabu wenye nguvu tetemeko limewapata, Watu wote wakaao Kanaani wameyeyuka.

16Hofu na woga umewaangukia; Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe; Hata watakapovuka watu wako, Ee Bwana, Hata watakapovuka watu wako uliowanunua.

17Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee Bwana, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, Bwana, kwa mikono yako.

18Bwana atatawala milele na milele.

19Kwa maana farasi za Farao na magari yake na wapanda farasi wake waliingia ndani ya bahari, Bwana akayarudisha maji ya bahari juu yao; bali wana wa Israeli walikwenda katika nchi kavu katikati ya bahari.

20Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza.

21Miriamu akawaitikia,

22Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.

23Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara.

24Ndipo watu wakamnung'unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?

25Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko;

26akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.

27Wakafikilia Elimu, palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na mitende sabini; wakapanga hapo, karibu na maji.