Kutoka - Sura ya 21

1Basi hukumu utakazoziweka mbele ya watu ni hizi
2Ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia muda wa miaka sita; mwaka wa saba atatoka kwako huru bure.
3Kwamba aliingia kwako peke yake tu, atatoka hivyo peke yake; kwamba ameoa, mkewe atatoka aende pamoja naye.
4Kwamba ni bwana wake aliyempa huyo mke, naye amemzalia wana, wa kiume au wa kike; yule mke na wanawe watakuwa ni mali ya bwana wake, naye mume atatoka peke yake.
5Lakini huyo mtumwa akisema waziwazi, Mimi nampenda bwana wangu, na mke wangu na watoto wangu; sitaki mimi kutoka niwe huru;
6ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya Mungu na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake atalitoboa sikio lake kwa uma; ndipo atamtumikia sikuzote.
7Mtu akimwuza binti yake awe kijakazi, hatatoka yeye kama watumwa wa kiume watokavyo.
8Kwamba bwana wake hakupendezewa naye, akiwa amemposa, ndipo atakubali akombolewe; hana amri yeye kumwuza aende kwa watu wageni maana amemtenda kwa udanganyifu.
9Kwamba amposa mwanawe, atamtendea kama desturi zipasazo binti zake.
10Kwamba ajitwalia mke mwingine, chakula chake huyo, na nguo zake, na ngono yake, hatampunguzia.
11Kwamba hamfanyii mambo haya matatu, ndipo atatoka aende bure, pasipo kutolewa mali.
12Mtu awaye yote ampigaye mtu, hata akafa, hana budi atauawa huyo.
13Lakini kama hakumvizia, ila Mungu amemtia mkononi mwake; basi nitakuonyesha mahali atakapopakimbilia.
14Lakini, mtu akimwendea mwenziwe kwa kujikinai, kusudi apate kumwua kwa hila; huyo utamwondoa hata madhabahuni pangu, auawe.
15Ampigaye baba yake au mama yake, sharti atauawa.
16Yeye amwibaye mtu, na kumwuza, au akipatikana mkononi mwake, sharti atauawa huyo
17Yeye amwapizaye baba yake au mama yake, sharti atauawa.
18Watu wakigombana, na mmoja akimpiga mwenziwe kwa jiwe, au kwa konde, asife, lakini yualazwa kitandani mwake;
19atakapoinuka tena na kuenenda nje kwa kutegemea fimbo, ndipo hapo yule aliyempiga ataachwa; ila atamlipa kwa ajili ya hayo majira yake yaliyompotea, naye atamwuguza hata apone kabisa.
20Mtu akimpiga mtumwa wake, au kijakazi chake, kwa fimbo, naye akifa mkononi mwake, hana budi ataadhibiwa.
21Lakini akipona siku moja au mbili hataadhibiwa; maana, ni mali yake.
22Watu waume wakiteta pamoja, wakamwumiza mwanamke mwenye mimba hata akaharibu mimba, tena yasiwe madhara zaidi; sharti atatozwa mali kama atakavyomwandikia mumewe huyo mwanamke; atalipa kama hao waamuzi watakavyosema.
23Lakini kwamba pana madhara zaidi, ndipo utatoza uhai kwa uhai,
24jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu,
25kuteketeza kwa kuteketeza, jeraha kwa jeraha, chubuko kwa ajili ya chubuko.
26Mtu akimpiga mtumwa wake jicho, au jicho la kijakazi chake, na kuliharibu; atamwacha huru kwa ajili ya jicho lake.
27Au akimpiga mtumwa wake jino likang'oka, au jino la kijakazi chake, atamwacha huru kwa ajili ya jino lake.
28Ng'ombe akipiga pembe mtu mume au mtu mke, nao wakafa, huyo ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe, nyama yake isiliwe; lakini mwenye huyo ng'ombe ataachiliwa.
29Lakini kwamba huyo ng'ombe alizoea kupiga watu tangu hapo, naye mwenyewe ameonyeshwa jambo hilo, wala asimzuie, naye amemwua mtu mume au mwanamke; huyo ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe, na huyo mwenyewe naye atauawa.
30Lakini akiandikiwa ukombozi, ndipo atakapotoa kwa ajili ya uhai wake hicho atakachoandikiwa.
31Akiwa ng'ombe amempiga pembe mtoto wa kiume na kumtumbua, au akiwa amempiga mtoto wa kike, atatendwa kama hukumu hiyo.
32Ng'ombe akimtumbua mtumwa mume au kijakazi; mwenye ng'ombe atampa bwana wao shekeli thelathini za fedha, naye ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe.
33Kwamba mtu atafunua shimo, au kuchimba shimo, naye asilifunike, kisha ikawa ng'ombe au punda kutumbukia humo,
34mwenye shimo atalipa; atampa huyo mwenye mnyama fedha, na mnyama aliyekufa atakuwa ni wake.
35Ng'ombe wa mtu akimwumiza ng'ombe wa mtu mwingine hata akafa; ndipo watamwuza huyo ng'ombe aliye hai na kugawanya thamani yake; na ng'ombe aliyekufa pia watamgawanya.
36Au kwamba ilijulikana ya kuwa ng'ombe tangu hapo amezoea kupiga kwa pembe, wala mwenyewe asimzuie; ndipo atakapolipa yeye, ng'ombe kwa ng'ombe, na huyo ng'ombe aliyekufa atakuwa ni wake.