Kutoka - Sura ya 22

Kutoka - Sura ya 22

1Mtu akiiba ng'ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng'ombe watano badala ya ng'ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja.

2Mwivi akipatikana akiwa yu hali ya kuvunja mahali, naye akapigwa hata akafa, hapatakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake.

3Lakini kama jua limekucha juu yake, ndipo patakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake; ingempasa kutoa malipo kamili; akiwa hana kitu, na auzwe kwa ajili ya wivi wake.

4Kama hicho kitu kilichoibwa chapatikana hai mkononi mwake, kama ni ng'ombe, au punda, au kondoo; atalipa thamani yake mara mbili.

5Mtu akilisha katika shamba, au shamba la mizabibu, akimwacha mnyama wake, akala katika shamba la mtu mwingine; atalipa katika vitu vilivyo vizuri vya shamba lake mwenyewe, au vya mizabibu yake.

6Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa.

7Mtu akimpa mwenziwe amana ya fedha au vitu vingine amtunzie, na vitu vile vikaibwa katika nyumba ya mtu huyo; mwivi akipatikana, atalipa thamani yake mara mbili.

8Mwivi asipopatikana, ndipo mwenye nyumba atakaribia mbele ya Mungu, ionekane kwamba si yeye aliyetia mkono na kutwaa vyombo vya mwenziwe.

9Kila jambo la kukosana, kama ni la ng'ombe, au la punda, au la kondoo, au la mavazi, au la kitu cho chote kilichopotea, ambacho mtu mmoja asema ni chake, hilo jambo la watu wote wawili litaletwa mbele ya Mungu; na yeye atakayehukumiwa na Mungu kuwa ni mkosa atamlipa mwenziwe thamani yake mara mbili.

10Mtu akimpa mwenziwe punda, au ng'ombe, au kondoo, au mnyama ye yote, ili amtunzie; yule mnyama akafa, au akaumia, au akachukuliwa mtu asione;

11patakuwa na kiapo cha Bwana katikati ya watu hao wawili, kwamba alipeleka mkono wake kutwaa mali ya mwenziwe, na mwenyewe atakubali hayo, wala hatalipa.

12Lakini kwamba aliibiwa mnyama huyo, sharti amlipe yule mwenyewe.

13Kwamba aliraruliwa na mnyama mkali, na amlete uwe ushahidi; hatalipa kwa ajili ya mnyama aliyeraruliwa.

14Mtu akiazima mnyama kwa mwenziwe, naye akaumia huyo mnyama, au akafa, mwenyewe asipokuwapo, lazima atalipa.

15Kama huyo mwenyewe alikuwapo pamoja na mnyama wake, hatalipa; kama ni mnyama aliyeajiriwa, alikwenda kwa ajili ya ujira wake.

16Mtu akimshawishi mwanamwali, aliyeposwa na mume, na kulala naye, lazima atatoa mahari kwa ajili yake ili awe mkewe.

17Ikiwa baba yake huyo mwanamwali akataa kabisa kumpa, atalipa fedha kama hesabu ya mahari ya mwanamwali ilivyo.

18Usimwache mwanamke mchawi kuishi.

19Mtu awaye yote alalaye na mnyama sharti atauawa.

20Mtu atakayemchinjia sadaka mungu ye yote, isipokuwa ni yeye Bwana peke yake, na angamizwe kabisa.

21Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.

22Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima.

23Ukiwatesa watu hao katika neno lo lote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao,

24na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima.

25Ukimkopesha mtu aliye maskini, katika watu wangu walio pamoja nawe; usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia faida.

26Ikiwa wewe kwa njia yo yote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima utamrudishia mbele ya jua kuchwa;

27maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake; je! Atalalia nini? Itakuwa, hapo atakaponililia mimi, nitasikia; kwa kuwa mimi ni mwenye rehema.

28Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa watu wako.

29Usikawie kuleta malimbuko ya matunda yako na ya vinywaji vyako. Mzaliwa wa kwanza katika wanao waume utanipa mimi.

30Nawe utafanya vivyo katika ng'ombe zako, na kondoo zako; utamwacha siku saba pamoja na mama yake; siku ya nane utanipa mimi.

31Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yo yote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo.