Kutoka - Sura ya 28

Kutoka - Sura ya 28

1Nawe umlete Haruni ndugu yako karibu nami, na wanawe pamoja naye, miongoni mwa wana wa Israeli, ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Haruni, na Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari, wana wa Haruni.

2Nawe utamfanyia Haruni ndugu yako mavazi matakatifu, kwa utukufu na kwa uzuri.

3Nawe utawaambia watu wote wenye moyo wa hekima, niliowajaza na roho ya hekima wamfanyie Haruni mavazi ili kumtakasa anitumikie katika kazi ya ukuhani.

4Na mavazi watakayoyafanya ni haya; kifuko cha kifuani, na naivera, na joho, na kanzu ya kazi ya urembo; na kilemba, na mshipi; nao watawafanyia Haruni nduguyo, na wanawe, mavazi matakatifu ili anitumikie katika kazi ya ukuhani.

5Nao wataitwaa dhahabu, na nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu, na nguo ya kitani nzuri.

6Nao waifanye naivera kwa nyuzi za dhahabu, na za samawi, na za zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa kwa kazi ya mstadi.

7Itakuwa na vipande viwili vya mabegani, vilivyoungana kwenye ncha zake mbili; ili ipate kuunganywa.

8Na mshipi wa kazi ya ustadi ulio juu yake, ili kuifunga mahali pake; utakuwa wa kazi kama ile ya naivera, ya vitu vile vile ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa.

9Nawe utatwaa vito viwili vya shohamu, ya rangi ya chani-kiwiti, nawe utachora juu yake majina ya wana wa Israeli;

10majina yao sita katika kito kimoja, na majina sita yaliyosalia katika kile kito cha pili, kwa utaratibu wa kuzaliwa kwao.

11Kwa kazi mtu mwenye kuchora mawe kama vile muhuri ichorwavyo, utavichora hivi vito viwili, sawasawa na majina ya wana wa Israeli, nawe utavitia katika vijalizo vya dhahabu.

12Nawe utavitia vile vito viwili juu ya vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli; naye Haruni atayachukua majina yao mbele za Bwana juu ya mabega yake mawili ili kuwa ukumbusho.

13Nawe fanya vijalizo viwili vya dhahabu;

14na mikufu miwili ya dhahabu safi; utaifanya iwe mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa; nawe uitie ile mikufu ya kazi ya kusokotwa katika vile vijalizo.

15Nawe utafanya kifuko cha kifuani cha hukumu, kazi ya fundi stadi; utakifanya kwa kuiandama ile kazi ya hiyo naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani safi yenye kusokotwa, ndivyo utakavyokifanya.

16Kitakuwa mraba, tena cha kukunjwa; urefu wake utakuwa shibiri moja, na upana wake shibiri moja.

17Nawe ukijaze viweko vya vito, safu nne za vito; safu moja itakuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, hivi vitakuwa safu ya kwanza;

18na safu ya pili itakuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi;

19na safu ya tatu itakuwa hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto;

20na safu ya nne itakuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi; vito hivyo vitakazwa ndani ya dhahabu kwa kujaa mahali pake.

21Na vile vito vitakuwa sawasawa na majina ya wana wa Israeli, kumi na viwili, sawasawa na majina yao; mfano wa kuchora kwa muhuri kila kimoja sawasawa na jina lake, vitakuwa vya hizo kabila kumi na mbili.

22Nawe utie katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa, ya dhahabu safi.

23Nawe utie pete mbili za dhahabu katika kile kifuko cha kifuani, na kuzitia hizo pete mbili katika ncha mbili za kifuko cha kifuani.

24Nawe utie hiyo mikufu miwili ya dhahabu iliyosokotwa katika zile pete mbili zilizo katika ncha za kifuko cha kifuani.

25Na ncha zile nyingine za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa utazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera upande wa mbele.

26Nawe utafanya pete mbili za dhahabu, uzitie katika hizo ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani.

27Nawe fanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya mabegani vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi.

28Nao watakikaza kile kileso kwa zile pete zake kwenye pete za naivera kwa ukanda wa rangi ya samawi, ili kwamba kikae pale juu ya ule mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, ili kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera.

29Na Haruni atayachukua majina ya wana wa Israeli katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu juu ya moyo wake, hapo atakapoingia ndani ya mahali patakatifu, kuwa ukumbusho mbele ya Bwana daima.

30Nawe utie hizo Urimu na Thumimu katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu; nazo zitakuwa juu ya moyo wa Haruni, hapo atakapoingia ndani mbele ya Bwana; na Haruni atachukua hukumu ya hao wana wa Israeli juu ya moyo wake mbele ya Bwana daima.

31Nawe fanya hiyo joho ya naivera ya rangi ya samawi yote.

32Nayo itakuwa na tundu katikati yake kwa kupitisha kichwa; itakuwa na utepe wa kazi ya kusokotwa kuzunguka hilo tundu lake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, ili lisipasuke.

33Nawe katika pindo zake utatia makomamanga ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu, kuzunguka pindo zake kotekote; na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga pande zote;

34njuga ya dhahabu na komamanga, njuga ya dhahabu na komamanga, katika pindo za joho kuizunguka pande zote.

35Nayo itakuwa juu ya Haruni akitumika; na sauti ya hizo njuga itasikilikana hapo aingiapo ndani ya mahali patakatifu mbele ya Bwana na hapo atokapo nje, ili kwamba asife.

36Nawe fanya bamba la dhahabu safi na kuchora juu yake, mfano wa machoro ya muhuri, MTAKATIFU KWA Bwana.

37Nawe ulitie hilo bamba katika ukanda wa rangi ya samawi, nalo litakuwa katika kile kilemba; litakuwa upande wa mbele wa kile kilemba.

38Nalo litakuwa katika kipaji cha uso cha Haruni, na Haruni atauchukua uovu wa vile vitu vitakatifu, watakavyovitakasa hao wana wa Israeli katika vipawa vyao vyote vitakatifu, nalo litakuwa katika kipaji chake cha uso sikuzote, ili kwamba vipate kukubaliwa mbele za Bwana.

39Na hiyo kanzu utaifuma ya kitani nzuri ya kazi ya urembo, ufanye na kilemba cha nguo ya kitani nzuri, nawe utafanya mshipi wa kazi ya mwenye kutia taraza.

40Kisha utafanya kanzu kwa ajili ya wana wa Haruni, nawe wafanyie mishipi, wafanyie na kofia kwa utukufu na uzuri.

41Nawe mvike huyo nduguyo Haruni na wanawe nao mavazi hayo; nawe watie mafuta, na kuwaweka kwa kazi takatifu, na kuwatakasa, ili wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani.

42Nawe wafanyie suruali za nguo ya kitani, ili kufunika tupu ya miili yao; suruali hizo zitafika tangu kiunoni hata mapajani;

43na Haruni na wanawe watazivaa, hapo watakapoingia katika hema ya kukutania, au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike katika mahali patakatifu; wasije wakachukua uovu, wakafa; hii itakuwa ni amri ya milele kwake yeye, na kwa wazao wake.