Kutoka - Sura ya 29

Kutoka - Sura ya 29

1Nawe uwafanyie jambo hili, ili kuwatakasa, wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani; twaa ng'ombe mmoja mume kijana, na kondoo waume wawili walio wakamilifu,

2na mkate usiotiwa chachu, na maandazi yasiyotiwa chachu yaliyokandwa kwa mafuta, na kaki zisizotiwa chachu zilizotiwa mafuta; utazifanya za unga mzuri mwembamba wa ngano.

3Nawe vitie vyote katika kikapu, uvilete ndani ya kikapu, pamoja na huyo ng'ombe, na hao kondoo waume wawili.

4Kisha mlete Haruni na wanawe hata mlangoni pa hema ya kukutania, ukawaoshe kwa maji.

5Kisha twaa hayo mavazi na kumvika Haruni; itie kanzu, na joho ya naivera, na naivera, na kifuko cha kifuani, na kumkaza kwa huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi;

6nawe mvike kile kilemba kichwani, na ile taji takatifu utaitia katika kile kilemba.

7Ndipo utakapotwaa hayo mafuta ya kutiwa, na kummiminia kichwani mwake, na kumtia mafuta.

8Kisha walete hao wanawe na kuwavika kanzu.

9Nawe uwakaze mishipi, Haruni na wanawe, na kuwavika kofia; nao watakuwa na huo ukuhani kwa amri ya milele; nawe utawaweka Haruni na wanawe kwa kazi takatifu.

10Kisha utamleta huyo ng'ombe mbele ya hema ya kukutania; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo ng'ombe.

11Kisha utamchinja huyo ng'ombe mbele ya Bwana, mlangoni pa hema ya kukutania.

12Kisha twaa baadhi ya damu ya ng'ombe, uitie katika pembe za madhabahu kwa kidole chako; na kuimimina damu yote chini ya madhabahu.

13Kisha twaa mafuta yote yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo juu yake, uyateketeze yote juu ya madhabahu.

14Lakini nyama yake huyo ng'ombe, na ngozi yake, na mavi yake, utayachoma kwa moto nje ya marago; ni sadaka kwa ajili ya dhambi.

15Pia mtwae kondoo mume mmoja; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo mume.

16Kisha utamchinja huyo kondoo mume, na kuitwaa damu yake, na kuinyunyiza katika madhabahu kuizunguka kando-kando.

17Kisha utamkata-kata kondoo vipande vyake, na kuyaosha matumbo yake na miguu yake, na kuiweka pamoja na vipande vyake na kichwa chake.

18Nawe mteketeze kondoo mzima juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya Bwana; ni harufu nzuri, sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.

19Kisha mtwae huyo kondoo wa pili; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo.

20Kisha utamchinja kondoo, na kuitwaa damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la Haruni la upande wa kuume, na katika ncha za masikio ya kuume ya wanawe, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vikuu vya miguu yao ya kuume, na kuinyunyiza hiyo damu katika madhabahu kuizunguka kando-kando.

21Kisha twaa katika hiyo damu iliyo juu ya madhabahu, na katika hayo mafuta ya kutiwa, na kumnyunyizia Haruni, juu ya mavazi yake, na wanawe, na mavazi yao pia, pamoja naye; naye atatakaswa, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye.

22Tena yatwae mafuta ya huyo kondoo mume, na mkia wake wa mafuta, na mafuta yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo katika hizo figo, na paja la kuume; kwani ni kondoo ambaye ni wa kuwekwa kwa kazi takatifu;

23utwae na mkate mmoja wa unga, na mkate mmoja ulioandaliwa kwa mafuta, na kaki moja katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichowekwa mbele ya Bwana;

24nawe utavitia hivi vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe; nawe utavitikisa-tikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana.

25Kisha uvitwae vile vitu mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri mbele ya Bwana; ni sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.

26Kisha twaa kidari cha huyo kondoo wa kuwekwa kwake Haruni kwa kazi takatifu, na kukitikisa-tikisa kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; nacho kitakuwa ni sehemu yako.

27Nawe kitakase kile kidari cha ile sadaka ya kutikiswa, na lile paja la sadaka ya kuinuliwa, lililotikiswa, na lililoinuliwa juu, vya yule kondoo wa kuwekwa kwa kazi takatifu, huyo aliyekuwa kwa ajili ya Haruni, na huyo aliyekuwa kwa ajili ya wanawe;

28navyo vitakuwa vya Haruni na wanawe posho ya lazima sikuzote itokayo kwa hao wana wa Israeli; kwa kuwa ni sadaka ya kuinuliwa; nayo itakuwa ni sadaka ya kuinuliwa itokayo kwa hao wana wa Israeli katika dhabihu zao za sadaka za amani, ni sadaka yao ya kuinuliwa kwa ajili ya Bwana.

29Na hayo mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wanawe baada yake, wayavae watakapotiwa mafuta, na watakapowekwa kwa kazi takatifu.

30Huyo mwanawe atakayekuwa kuhani badala yake atayavaa muda wa siku saba, hapo atakapoingia ndani ya hiyo hema ya kukutania, ili atumike ndani ya mahali patakatifu.

31Nawe twaa huyo kondoo mume aliyekuwa wa kuwekwa kwa kazi takatifu, na kuitokosa nyama yake katika mahali patakatifu.

32Na Haruni na wanawe wataila ile nyama ya kondoo, na mikate iliyo katika kile kikapu, hapo mbele ya mlango wa hema ya kukutania.

33Nao watakula vile vitu ambavyo upatanisho ulifanywa kwa hivyo, ili kuwaweka kwa kazi takatifu na kuwatakasa; lakini mgeni asivile, maana, ni vitu vitakatifu.

34Na kwamba kitu cho chote cha ile nyama, iliyo kwa ajili ya kuweka kwa kazi takatifu, au cho chote cha hiyo mikate, kikisalia hata asubuhi, ndipo utavichoma kwa moto hivyo vilivyosalia; havitaliwa, maana, ni vitu vitakatifu.

35Ni hivyo utakavyowatendea Haruni na wanawe, sawasawa na hayo yote niliyokuagiza; utawaweka kwa kazi takatifu siku saba.

36Kila siku utamtoa ng'ombe wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya upatanisho; nawe utaisafisha hiyo madhabahu, hapo utakapofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu; nawe utaitia mafuta, ili kuitakasa.

37Utafanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu muda wa siku saba, na kuitakasa; ndipo madhabahu itakapokuwa takatifu sana; kila kitu kiigusacho madhabahu kitakuwa kitakatifu.

38Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku daima.

39Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni;

40tena, pamoja na mwana-kondoo mmoja utatoa vibaba vitatu vya unga mzuri uliochanganyika na mafuta yenye kupondwa, kiasi cha kibaba na robo kibaba; na divai kiasi cha kibaba na robo kibaba, iwe sadaka ya kinywaji.

41Na huyo mwana-kondoo wa pili utamchinja wakati wa jioni, nawe utamfanyia vivyo kama ile sadaka ya unga ya asubuhi, na kama ile sadaka yake ya kinywaji, iwe harufu nzuri, ni dhabihu ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.

42Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya Bwana; hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo.

43Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo, na hiyo Hema itafanywa takatifu na utukufu wangu.

44Nami nitaitakasa hiyo hema ya kukutania, na hiyo madhabahu; pia Haruni na wanawe nitawatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.

45Na mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao.

46Nao watanijua kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wao, niliyewaleta watoke katika nchi ya Misri, nipate kukaa kati yao; ni mimi Bwana Mungu wao.