Kutoka - Sura ya 32

Kutoka - Sura ya 32

1Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata.

2Haruni akawaambia, Zivunjeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mkaniletee.

3Watu wote wakazivunja pete za dhahabu zilizo katika masikio yao, wakamletea Haruni.

4Akaipokea mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha; nao wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri.

5Naye Haruni alipoona jambo hili, akajenga madhabahu mbele yake; Haruni akatangaza akasema, Kesho itakuwa sikukuu kwa Bwana.

6Wakaondoka asubuhi na mapema, wakatoa dhabihu, wakaleta sadaka za amani, watu wakaketi kula na kunywa, wakaondoka wacheze.

7Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao,

8wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri.

9Tena Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu

10basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu.

11Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu?

12Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako.

13Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele.

14Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.

15Basi, Musa akageuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao zilizoandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa.

16Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao.

17Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita maragoni.

18Akasema, Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao ndizo ninazozisikia mimi.

19Hata alipoyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima.

20Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli.

21Musa akamwambia Haruni Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao?

22Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake, wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya.

23Maana waliniambia, Katufanyie miungu, itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata.

24Nikawaambia, Mtu ye yote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu.

25Basi Musa alipoona ya kuwa watu hawa wameasi, maana Haruni amewaacha waasi, ili wawe dhihaka kati ya adui zao,

26ndipo Musa akasimama katika mlango wa marago, akasema, Mtu awaye yote aliye upande wa Bwana, na aje kwangu. Wana wa Lawi wote wakamkusanyikia

27Akawaambia, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila mtu na ajifunge upanga wake pajani mwake, akapite huko na huko toka mlango hata mlango kati ya marago, mkamchinje kila mtu ndugu yake, na kila mtu mwenziwe na kila mtu jirani yake.

28Na hao wana wa Lawi wakafanya kama vile alivyosema Musa, wakaanguka siku ile kama watu elfu tatu.

29Musa akasema, Jiwekeni wakfu kwa Bwana leo, naam, kila mtu juu ya mwanawe na juu ya ndugu yake; ili awape baraka leo.

30Hata asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa Bwana, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.

31Musa akarejea kwa Bwana akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu.

32Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao -- na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika.

33Bwana akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu.

34Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekwambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.

35Bwana akawapiga hao watu, kwa walivyoifanya ile ndama, ambayo Haruni aliifanya.