Kutoka - Sura ya 34

Kutoka - Sura ya 34

1Kisha Bwana akamwambia Musa, Chonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza; nami nitaandika juu ya mbao hizo maneno hayo yaliyokuwa juu ya mbao za kwanza, hizo ulizozivunja.

2Nawe uwe tayari asubuhi, na asubuhi ukwee juu katika mlima wa Sinai, nawe hudhurisha nafsi yako kwangu huko katika kilele cha mlima.

3Asikwee mtu pamoja nawe, wala asionekane mtu awaye yote katika huo mlima; wala kondoo na ng'ombe wasilishe mbele ya huo mlima.

4Naye akachonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza; na Musa akainuka na mapema asubuhi, naye akakwea katika mlima wa Sinai, kama Bwana alivyomwamuru, akazichukua hizo mbao mbili za mawe mkononi mwake.

5Bwana akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la Bwana.

6Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli;

7mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.

8Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu.

9Akasema, Ikiwa sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu, maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako.

10Akasema, Tazama, nafanya agano; mbele ya watu wangu wote nitatenda miujiza, ya namna isiyotendeka katika dunia yote, wala katika taifa lo lote; na watu wote ambao unakaa kati yao wataona kazi ya Bwana, kwa maana ni neno la kutisha nikutendalo.

11Liangalie neno hili ninalokuamuru leo; tazama, mbele yako namtoa Mwamori, na Mkanaani, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.

12Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako.

13Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao.

14Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa Bwana, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu.

15Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake.

16Ukawaoza wana wako binti zao, nao binti zao wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, wakawavuta wana wenu wafanye uzinzi na miungu yao.

17Usijifanyizie miungu ya kuyeyusha.

18Hiyo sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu utaitunza. Utakula mikate isiyotiwa chachu muda wa siku saba, kama nilivyokuagiza, kwa majira yaliyoaganwa katika mwezi wa Abibu; kwa kuwa ulitoka Misri katika mwezi huo wa Abibu.

19Kila kifunguacho mimba ni changu mimi; na wanyama wako wote walio waume, wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na wa kondoo.

20Na mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo; tena kwamba hutaki kumkomboa, ndipo utamvunja shingo. Wazaliwa wa kwanza wote wa wanao utawakomboa. Wala hapana atakayehudhuria mbele zangu mikono mitupu.

21Utafanya kazi siku sita, lakini katika siku ya saba utapumzika; wakati wa kulima mashamba, na wakati wa kuvuna pia, utapumzika.

22Nawe utaitunza sikukuu ya majuma, nayo ni ya malimbuko ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya vitu mwisho wa mwaka.

23Mara tatu kila mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele za Bwana MUNGU, Mungu wa Israeli.

24Kwa kuwa mimi nitazitupa nje taifa za watu mbele yako, na kuipanua mipaka yako; wala hapana mtu ye yote atakayeitamani nchi yako, hapo utakapokwea kwenda kuhudhuria mbele za Bwana Mungu wako mara tatu kila mwaka.

25Usisongeze damu ya sadaka yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu; wala hiyo sadaka ya sikukuu ya pasaka haitasazwa hata asubuhi.

26Vitu vya kwanza vya malimbuko ya nchi yako utavileta na kuvitia ndani ya nyumba ya Bwana Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.

27Bwana akamwambia Musa, Andika maneno haya; kwa kuwa mimi nimefanya agano nawe, na pamoja na Israeli, kwa mujibu wa maneno haya.

28Naye alikuwa huko pamoja na Bwana siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.

29Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling'aa kwa sababu amesema naye.

30Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling'aa; nao wakaogopa kumkaribia.

31Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao.

32Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo Bwana amemwambia katika mlima Sinai.

33Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake.

34Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za Bwana kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa.

35Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling'aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.