Kutoka - Sura ya 36

Kutoka - Sura ya 36

1Basi Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye Bwana amemtia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa huo utumishi wa mahali patakatifu, kama hayo yote Bwana aliyoyaagiza.

2Basi Musa akawaita Bezaleli na Oholiabu, na kila mtu aliyekuwa na moyo wa akili, ambaye Bwana alimtia moyoni mwake hekima, kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza ili aende kuifanya kazi hiyo;

3nao wakapokea mkononi mwa Musa matoleo yote, ambayo hao wana wa Israeli walikuwa wameyaleta kwa ajili ya huo utumishi wa mahali patakatifu, ili wapafanye. Kisha wakamletea matoleo kila siku asubuhi kwa moyo wa kupenda.

4Na hao watu wote wenye hekima, waliotumika katika kazi yote ya mahali patakatifu, wakaenda kila mtu kutoka katika kazi yake aliyokuwa akiifanya;

5nao wakasema na Musa, na kumwambia, Watu waleta vitu vingi sana zaidi ya hivyo vitoshavyo kwa ajili ya utumishi wa hiyo kazi, ambayo Bwana aliagiza ifanywe.

6Basi Musa akatoa amri, nao wakatangaza mbiu katika marago yote, wakisema, Wasifanye kazi tena, mtu mume wala mwanamke, kwa ajili ya matoleo kwa mahali patakatifu. Basi watu wakazuiwa wasilete tena.

7Kwani vile vitu walivyokuwa navyo vilikuwa vyatosha kwa kuifanya kazi hiyo yote, kisha vilizidi.

8Basi kila mtu mwenye moyo wa hekima miongoni mwa hao waliofanya kazi, akaifanya hiyo maskani ya mapazia kumi; ya nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu; pamoja na makerubi, kazi ya fundi stadi; ndivyo alivyoyafanya.

9Urefu wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa ishirini na nane, na upana wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa nne; mapazia yote yalikuwa ya kipimo kimoja.

10Naye akaunganisha mapazia matano hili na hili; na mapazia matano mengine akayaunganisha hili na hili.

11Kisha akafanya matanzi ya rangi ya samawi katika ncha za pazia moja, katika upindo wa kiungo chake; akafanya vivyo katika ncha ya pazia lililokuwa upande wa nje katika kiungo cha pili.

12Akafanya matanzi hamsini katika pazia moja, na matanzi hamsini katika upindo wa pazia lililokuwa katika kiungo cha pili; hayo matanzi yalikuwa yakabiliana hili na hili.

13Kisha akafanya vifungo hamsini vya dhahabu, na kuyaunganya hayo mapazia hili na hili kwa vile vifungo; hivi ile maskani ilikuwa ni moja.

14Kisha akafanya vifuniko vya singa za mbuzi kuwa hema ya kuifunika hiyo maskani; akafanya mapazia kumi na moja.

15Urefu wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa thelathini, na upana wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa nne; hayo mapazia yote kumi na moja yalikuwa ya kipimo kimoja.

16Naye akaunganya mapazia matano mbali, na mapazia sita mbali.

17Kisha akafanya matanzi hamsini katika upindo wa pazia lililo upande wa nje katika kile kiungo, naye akafanya matanzi hamsini katika ncha ya pazia lililokuwa upande wa nje katika kiungo cha pili.

18Kisha akafanya vifungo hamsini vya shaba aiunganye ile hema pamoja, ili iwe hema moja.

19Kisha akafanya kifuniko kwa ajili ya hiyo hema cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu; tena juu yake akafanya kifuniko cha ngozi za pomboo.

20Kisha akafanya mbao za mti wa mshita kwa hiyo maskani, zilizosimama.

21Urefu wa kila ubao ulikuwa ni dhiraa kumi, na upana wa kila ubao ulikuwa ni dhiraa moja na nusu.

22Kila ubao ulikuwa na ndimi mbili, zilizounganywa pamoja; ndivyo alivyozifanya hizo mbao zote za maskani.

23Naye akazifanya hizo mbao kwa ajili ya hiyo maskani; mbao ishirini kwa upande wa kusini kuelekea kusini;

24naye akafanya matako ya fedha arobaini yawe chini ya hizo mbao ishirini; matako mawili chini ya ubao mmoja kwa hizo ndimi zake mbili, na matako mawili chini ya ubao mwingine kwa ndimi zake mbili.

25Na kwa upande wa pili wa maskani upande wa kaskazini, akafanya mbao ishirini,

26na matako yake ya fedha arobaini; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao mwingine.

27Na kwa upande wa nyuma wa hiyo maskani kuelekea magharibi akafanya mbao sita.

28Naye akafanya mbao mbili kwa pembe za maskani upande wa nyuma.

29Nazo zilikuwa mbao pacha upande wa chini, vivyo zilishikamana pamoja hata ncha ya juu kufikilia pete ya kwanza; ndivyo alivyofanya zote mbili katika hizo pembe mbili.

30Hivyo zilikuwa mbao nane, na matako yake ya fedha, matako kumi na sita, matako mawili chini ya kila ubao.

31Kisha akafanya mataruma ya miti ya mshita; matano kwa mbao za upande mmoja wa maskani;

32na mataruma matano kwa mbao za upande wa pili wa maskani, na mataruma matano kwa hizo mbao za maskani zilizokuwa upande wa nyuma kuelekea magharibi.

33Naye akalifanya hilo taruma la katikati lipenye kati ya hizo mbao kutoka upande huu hata upande huu.

34Naye akazifunika hizo mbao dhahabu, akazifanya zile pete zake za dhahabu ziwe mahali pa hayo mataruma, akayafunika dhahabu hayo mataruma.

35Kisha akafanya hilo pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri zilizosokotwa; akatia na makerubi kazi ya fundi stadi, ndivyo alivyofanya.

36Naye akafanya kwa ajili yake nguzo nne za mti wa mshita, akazifunika dhahabu; na kulabu zake zilikuwa za dhahabu; naye akasubu kwa ajili yake matako manne ya fedha.

37Kisha akafanya pazia la sitara kwa ajili ya mlango wa Hema, la nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na nyekundu, na nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, kazi ya mwenye kutia taraza,

38na nguzo zake tano pamoja na kulabu zake; naye akavifunika dhahabu vichwa vyake na vifungo vyake; na matako yake matano yalikuwa ya shaba.