Kutoka - Sura ya 5

Kutoka - Sura ya 5

1Hata baadaye, Musa na Haruni wakaenda wakamwambia Farao, wakasema, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Wape watu wangu ruhusa waende, ili kunifanyia sikukuu jangwani.

2Farao akasema, Bwana ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui Bwana, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao.

3Wakasema, Mungu wa Waebrania amekutana nasi; twakuomba, tupe ruhusa twende safari ya siku tatu jangwani, tumtolee dhabihu Bwana, Mungu wetu; asije akatupiga kwa tauni, au kwa upanga.

4Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu kazi zao? Enendeni zenu kwa mizigo yenu.

5Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao.

6Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema,

7Msiwape watu tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende wakatafute majani wenyewe.

8Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.

9Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya uongo.

10Hao wasimamizi wa watu na wanyapara wao wakatoka, wakasema na watu, wakanena, Farao asema hivi, Mimi siwapi majani.

11Enendeni wenyewe, jipatieni majani hapo mtakapoyaona; kwa maana kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.

12Basi hao watu wakatawanyika katika nchi yote ya Misri ili wapate kukusanya matakataka ya mashamba badala ya majani.

13Wasimamizi wao wakawahimiza, wakisema, Timizeni kazi zenu, shughuli zenu za kila siku, kama wakati ule majani yalipokuwapo.

14Na wanyapara wa wana wa Israeli, ambao wasimamizi wa Farao wamewaweka juu yao, wakapigwa, wakiambiwa, Kwa nini hamkutimiza kazi yenu jana na leo; kwa kufanya matofali kama hapo kwanza?

15Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaenda, wakamlilia Farao, wakisema, Mbona umetutendea hivi, sisi watumwa wako?

16Watumwa wako hawapewi majani, nao wanatuambia, Fanyeni matofali; na tazama, watumwa wako wapigwa; lakini kosa hilo ni la watu wako mwenyewe.

17Akasema, Wavivu ninyi; wavivu; kwa ajili hii mwasema, Tupe ruhusa twende kumtolea Bwana dhabihu.

18Basi, enendeni sasa, mkafanye kazi; kwa maana hamtapewa majani, na pamoja na hayo mtaleta hesabu ile ile ya matofali.

19Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaona ya kwamba wa katika hali mbaya, walipoambiwa, Hamtapunguza hesabu ya matofali yenu hata kidogo; ndizo shughuli zenu za kila siku.

20Wakakutana na Musa na Haruni, waliokuwa wanasimama njiani, hapo walipotoka kwa Farao;

21wakawaambia, Bwana awaangalie na kuamua; kwa kuwa mmefanya harufu yetu kuwa chukizo mbele ya Farao, na mbele ya watumishi wake, mkatia upanga mikononi mwao, watuue.

22Musa akarudi kwa Bwana, akasema, Bwana, mbona umewatenda mabaya watu hawa? Kwani kunituma mimi?

23Kwa maana tangu nilipokwenda kwa Farao, kusema naye kwa jina lako, amewatenda mabaya watu hawa; wala hukuwaokoa watu wako hata kidogo.