Kutoka - Sura ya 6

Kutoka - Sura ya 6

1Bwana akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake.

2Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni YEHOVA;

3nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao.

4Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya kukaa kwao hali ya ugeni.

5Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu.

6Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa;

7nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri.

8Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo naliinua mkono wangu, niwape Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni YEHOVA.

9Musa akawaambia wana wa Israeli maneno haya; lakini hawakumsikiliza Musa kwa ajili ya uchungu wa moyo, na kwa ajili ya utumwa mgumu.

10Bwana akasema na Musa, akamwambia,

11Ingia ndani, ukaseme na Farao, mfalme wa Misri, ili awape ruhusa wana wa Israeli watoke nchi yake.

12Musa akanena mbele ya Bwana, akasema, Tazama, hao wana wa Israeli hawakunisikiza mimi; basi huyo Farao atanisikizaje, mimi niliye na midomo isiyo tohara?

13Bwana akanena na Musa na Haruni, akawaagiza wawaendee wana wa Israeli, na Farao, mfalme wa Misri, ili awatoe hao wana wa Israeli katika nchi ya Misri.

14Hawa ndio vichwa vya nyumba za baba zao: wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli; ni Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi; hao ni jamaa za Reubeni.

15Na wana wa Simeoni; ni Yemueli, na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli mwana wa mwanamke wa Kikanaani; hao ni jamaa za Simeoni.

16Na haya ndiyo majina ya wana wa Lawi, sawasawa na vizazi vyao; Gershoni, na Kohathi, na Merari; na miaka ya maisha yake Lawi ilikuwa ni miaka mia na thelathini na saba.

17Wana wa Gershoni; ni Libni, na Shimei, sawasawa na jamaa zao.

18Na wana wa Kohathi; ni Amramu, na Ishari, na Hebroni, na Uzieli; na miaka ya maisha ya huyo Kohathi ilikuwa ni miaka mia na thelathini na mitatu.

19Na wana wa Merari; ni Mali, na Mushi. Hizi ni jamaa za hao Walawi sawasawa na vizazi vyao.

20Huyo Amramu akamwoa Yokebedi ndugu ya baba yake; naye akamzalia Haruni, na Musa; na miaka ya maisha yake Amramu ilikuwa ni miaka mia na thelathini na saba.

21Na wana wa Ishari; ni Kora, na Nefegi, na Zikri.

22Na wana wa Uzieli; ni Mishaeli, na Elisafani, na Sithri.

23Haruni akamwoa Elisheba, binti ya Aminadabu, umbu lake Nashoni; naye akamzalia Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari.

24Na wana wa Kora; ni Asiri, na Elkana, na Abiasafu; hizo ni jamaa za hao Wakora.

25Na Eleazari mwana wa Haruni akamwoa mmoja miongoni mwa binti za Putieli; naye akamzalia Finehasi. Hawa ndio vichwa vya nyumba za mababa ya Walawi sawasawa na jamaa zao.

26Hawa ni Haruni ye yule, na Musa ye yule, Bwana aliowaambia, akisema, Watoeni wana wa Israeli watoke nchi ya Misri sawasawa na majeshi yao.

27Ni hao walionena na Farao mfalme wa Misri ili wawatoe wana wa Israeli watoke Misri; hao ni Musa ye yule, na Haruni ye yule.

28Ilikuwa siku hiyo Bwana aliponena na Musa katika nchi ya Misri,

29Bwana akamwambia Musa, akasema, Mimi ni Bwana; mwambie Farao mfalme wa Misri maneno yote nikuambiayo.

30Musa akanena mbele ya Bwana, Mimi ni mtu mwenye midomo isiyo tohara, Farao atanisikizaje?