Ezekieli - Sura ya 1

Ezekieli - Sura ya 1

1Ikawa katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa pamoja na watu waliohamishwa, karibu na mto Kebari, mbingu zilifunuka, nikaona maono ya Mungu.

2Siku ya tano ya mwezi, nao ulikuwa ni mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yehoyakini,

3neno la Bwana lilimjia Ezekieli, kuhani, mwana wa Buzi, kwa dhahiri, katika nchi ya Wakaldayo, karibu na mto Kebari; na mkono wa Bwana ulikuwa hapo juu yake.

4Nikaona, na tazama, upepo wa dhoruba ulitoka upande wa kaskazini, wingu kubwa sana, pamoja na moto, ukifanya duara ya nuru, na mwangaza pande zote, na katikati yake kitu kama rangi ya kaharabu, katikati ya moto huo.

5Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu.

6Na kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne.

7Na miguu yao ilikuwa miguu iliyonyoka; na nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za miguu ya ndama; zikimetameta kama rangi ya shaba iliyosuguliwa sana.

8Nao walikuwa na mikono ya mwanadamu chini ya mabawa yao, pande zote nne; na wote wanne walikuwa na nyuso zao na mabawa yao hivi;

9mabawa yao yaliungana, hili na hili; nao hawakugeuka walipokwenda, walikwenda kila mmoja kuelekea mbele.

10Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kuume; na hao wanne walikuwa na uso wa ng'ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia.

11Na nyuso zao na mabawa yao yalikuwa yametengana kwa juu; mabawa mawili ya kila mmoja yaliungana, hili na hili, na mawili yalifunika miili yao.

12Nao walikwenda kuelekea mbele, kila mmoja wao; roho ilikotaka kwenda ndiko walikokwenda; hawakugeuka walipokwenda.

13Kwa habari za kuonekana kwao vile viumbe hai; kuonekana kwao kulikuwa kama makaa ya moto yawakayo, kama kuonekana kwa vinga vya moto; moto ule ulikuwa ukienda juu na kushuka chini, katikati ya vile viumbe hai; na ule moto ulikuwa na mwangaza mwingi, na katika ule moto ulitoka umeme.

14Na vile viumbe hai walipiga mbio, kwenda na kurudi, kama kuonekana kwa kumulika kwa umeme.

15Basi, nilipokuwa nikivitazama vile viumbe hai, tazama, gurudumu moja juu ya nchi, karibu na kila kimoja cha vile viumbe hai, pande zake zote nne.

16Kuonekana kwake magurudumu hayo na kazi yake kulikuwa kama rangi ya zabarajadi; nayo yote manne yalikuwa na mfano mmoja; na kuonekana kwake na kazi yake kulikuwa kana kwamba ni gurudumu ndani ya gurudumu lingine.

17Yalipokwenda yalikwenda pande zote nne; hayakugeuka yalipokwenda.

18Katika habari za vivimbe vyake; vilikuwa virefu, vya kutisha; nayo yote manne, vivimbe vyake vimejaa macho pande zote.

19Na viumbe hao walipokwenda, magurudumu yalikwenda kandokando yao, na viumbe hao walipoinuliwa, magurudumu nayo yaliinuliwa.

20Kila mahali ambako roho hiyo ilitaka kwenda, walikwenda; walikuwa na roho ya kwenda huko; nayo magurudumu yaliinuliwa karibu nao; kwa maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu.

21Walipokwenda hao, yalikwenda hayo nayo; na waliposimama hao, yalisimama hayo nayo; na walipoinuliwa hao juu ya nchi, magurudumu yaliinuliwa karibu nao; maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu.

22Tena juu ya vichwa vya viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa anga, kama rangi ya bilauri, lenye kutisha, limetandwa juu ya vichwa vyao.

23Na chini ya anga mabawa yao yamenyoshwa, moja kulielekea la pili; kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande mmoja, na kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande wa pili.

24Nao walipokwenda nalisikia mshindo wa mabawa yao, kama mshindo wa maji makuu, kama sauti yake Mwenyezi, mshindo wa mvumo, kama mshindo wa jeshi; hapo waliposimama walishusha mabawa yao.

25Tena palikuwa na sauti juu ya anga lile, lililokuwa juu ya vichwa vyao; hapo waliposimama walishusha mabawa yao.

26Na juu ya anga, lililokuwa juu ya vichwa vyao, palikuwa na mfano wa kiti cha enzi, kuonekana kwake kama yakuti samawi; na juu ya mfano huo wa kiti cha enzi, ulikuwako mfano kama kuonekana kwa mfano wa mwanadamu juu yake.

27Nikaona kana kwamba ni rangi ya kaharabu, kama kuonekana kwa moto ndani yake pande zote, tangu kuonekana kwa viuno vyake na juu; na tangu kuonekana kwa viuno vyake na chini, naliona kana kwamba ni kuonekana kwa moto; tena palikuwa na mwangaza pande zake zote.

28Kama kuonekana kwa upinde wa mvua, ulio katika mawingu siku ya mvua, ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwa mwangaza ule pande zote. Ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwake mfano huo wa utukufu wa Bwana. Nami nilipoona nalianguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mmoja anenaye.