Ezekieli - Sura ya 13

Ezekieli - Sura ya 13

1Kisha neno la Bwana likanijia, kusema,

2Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri, uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, Lisikieni neno la Bwana;

3Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala hawakuona neno lo lote!

4Ee Israeli, manabii wako wamekuwa kama mbweha, mahali palipo ukiwa.

5Hamkupanda kwenda mahali palipobomolewa, wala hamkuitengenezea nyumba ya Israeli boma, wapate kusimama vitani katika siku ya Bwana.

6Wameona ubatili, na uganga wa uongo, hao wasemao, Bwana asema; lakini Bwana hakuwatuma; nao wamewatumainisha watu ya kuwa neno lile litatimizwa.

7Je! Hamkuona maono ya bure, hamkunena mabashiri ya uongo? Nanyi mwasema, Bwana asema; ila mimi sikusema neno.

8Basi tazama, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu mmenena ubatili, na kuona uongo, basi, kwa sababu hiyo, mimi ni juu yenu, asema Bwana MUNGU.

9Na mkono wangu utakuwa juu ya manabii wanaoona ubatili, na kutabiri uongo; hawatakuwa katika mashauri ya watu wangu, wala hawataandikwa katika maandiko ya nyumba ya Israeli, wala hawataingia katika nchi ya Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.

10Kwa sababu hiyo, kwa sababu wameshawishi watu wangu, wakisema, Amani; wala hapana amani; na mtu mmoja ajengapo ukuta, tazama, waupaka chokaa isiyokorogwa vema;

11basi waambie hao wanaoupaka ukuta chokaa isiyokorogwa vema, ya kwamba utaanguka; kutakuwa mvua ya kufurika; nanyi, enyi mvua ya mawe makubwa ya barafu, mtaanguka; na upepo wa dhoruba utaupasua.

12Na huo ukuta utakapoanguka, je! Hamtaambiwa, Ku wapi kupaka kwenu mlikoupaka?

13Basi Bwana MUNGU asema hivi; Nitaupasua kwa upepo wa dhoruba, katika ghadhabu yangu; tena kutakuwa mvua ya barafu ya kufurika katika hasira yangu; na mawe makubwa ya barafu katika hasira ya kuukomesha.

14Ndivyo nitakavyoubomoa ukuta mlioupaka chokaa isiyokorogwa vema, na kuuangusha chini, hata misingi yake itafunuliwa; nao utaanguka, nanyi mtaangamizwa katikati yake; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

15Ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu juu ya ukuta ule, na juu yao walioupaka chokaa isiyokorogwa vema; nami nitawaambieni, Ukuta huo hauko sasa, wala wao walioupaka hawako;

16yaani, manabii wa Israeli, watabirio habari za Yerusalemu, na kuona maono ya amani katika habari zake; wala hapana amani, asema Bwana MUNGU.

17Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao,

18useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe?

19Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo.

20Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege.

21Na leso zenu nazo nitazirarua, na kuwaokoa watu wangu katika mikono yenu, wala hawatakuwa katika mikono yenu tena kuwindwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

22Kwa kuwa ninyi mmemhuzunisha moyo mwenye haki kwa uongo, ambaye mimi sikumhuzunisha; na kuitia nguvu mikono ya mtu mbaya, hata asigeuke, na kuiacha njia yake mbaya, na kuhifadhika;

23basi, kwa sababu hiyo ninyi hamtaona tena ubatili, wala kutabiri mambo; nami nitawaokoa watu wangu katika mikono yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.