Ezekieli - Sura ya 22

Ezekieli - Sura ya 22

1Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

2Na wewe, mwanadamu, je! Utauhukumu, utauhukumu mji huu wa damu? Basi uujulishe machukizo yake yote.

3Nawe utasema, Bwana MUNGU asema hivi; Mji umwagao damu ndani yake, ili wakati wake upate kuja; mji ufanyao vinyago juu ya nafsi yake, ili ujitie unajisi!

4Umekuwa na hatia katika damu yako uliyomwaga, nawe umekuwa na unajisi kwa vinyago vyako ulivyovifanya; nawe umezileta karibu siku zako, nawe umefika karibu na miaka yako; basi, kwa sababu ya hayo, nimekufanya kuwa lawama kwa mataifa, na kuwa dhihaka katika nchi zote.

5Zilizo karibu, na zilizo mbali nawe, zitakudhihaki, Ewe mchafu, uliyejaa fujo.

6Tazama, wakuu wa Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya nguvu zake, wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu.

7Ndani yako wamedharau baba na mama; kati yako wamewatenda wageni udhalimu; ndani yako wamewaonea yatima na mjane.

8Umevidharau vitu vyangu vitakatifu, umezitia unajisi sabato zangu.

9Wasingiziaji wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu; na ndani yako wamekula juu ya milima; kati yako wamefanya uasherati.

10Ndani yako wamefunua uchi wa baba zao; ndani yako wamemfanyia nguvu mwanamke asiye safi wakati wa kutengwa kwake.

11Na mtu mmoja amefanya chukizo pamoja na mke wa jirani yake; na mtu mwingine amemharibu mke wa mwanawe kwa uasherati; na mtu mwingine ndani yako amemfanyia nguvu umbu lake, binti ya babaye.

12Ndani yako wamepokea rushwa ili kumwaga damu; umepokea riba na faida; nawe kwa choyo umepata mapato kwa kuwadhulumu jirani zako, nawe umenisahau mimi, asema Bwana MUNGU.

13Basi, tazama, nimeipigia kofi hiyo faida uliyopata kwa njia isiyo haki, na hiyo damu yako iliyokuwa kati yako.

14Je! Moyo wako waweza kuvumilia, au mkono wako waweza kuwa hodari, katika siku zile nitakapokutenda mambo? Mimi, Bwana, nimenena neno hili, tena nitalitenda.

15Nami nitakutawanya kati ya mataifa, na kukutapanya kati ya nchi mbalimbali; nami nitauteketeza uchafu wako, ili ukutoke.

16Nawe utatiwa unajisi ndani ya nafsi yako, mbele ya macho ya mataifa; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

17Neno la Bwana likanijia, kusema,

18Mwanadamu, nyumba ya Israeli imekuwa taka za fedha kwangu; wote wamekuwa shaba, na bati, na chuma, na risasi, kati ya tanuu; wamekuwa taka za fedha.

19Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu ninyi nyote mmekuwa taka za fedha, tazama, nitawakusanya kati ya Yerusalemu.

20Kama vile watu wakusanyavyo fedha, na shaba, na chuma, na risasi, na bati, kati ya tanuu, ili kuvifukutia moto na kuviyeyusha; ndivyo nitakavyowakusanya ninyi katika hasira yangu, na ghadhabu yangu, nami nitawalaza huko, na kuwayeyusha.

21Naam, nitawakusanya, na kuwafukutia moto wa ghadhabu yangu, nanyi mtayeyushwa kati yake.

22Kama fedha iyeyushwavyo kati ya tanuu, ndivyo mtakavyoyeyushwa kati yake; nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimemwaga ghadhabu yangu juu yenu.

23Neno la Bwana likanijia, kusema,

24Mwanadamu, uiambie nchi, Wewe u nchi isiyosafika, wala kunyeshewa mvua siku ya ghadhabu.

25Fitina ya manabii wake imo ndani yake, kama simba angurumaye akirarua mawindo; wamekula roho za watu; hutwaa kwa nguvu hazina na vitu vya thamani; wameongeza hesabu ya wajane wake ndani yake.

26Makuhani wake wameihalifu sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao.

27Wakuu wake kati yake wamekuwa kama mbwa-mwitu wakirarua mawindo; ili kumwaga damu, na kuharibu roho za watu, wapate faida kwa njia isiyo halali.

28Na manabii wake wamewapakia chokaa isiyokorogwa vema, wakiona ubatili, na kuwatabiria maneno ya uongo, wakisema, Bwana MUNGU asema hivi; iwapo Bwana hakusema neno.

29Watu wa nchi wametumia udhalimu, wamenyang'anya kwa nguvu; naam, wamewatenda jeuri maskini na wahitaji, nao wamewaonea wageni bila haki.

30Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.

31Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao; nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu; nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU.