Ezekieli - Sura ya 23

Ezekieli - Sura ya 23

1Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

2Mwanadamu, palikuwa na wanawake wawili, binti za mama mmoja;

3nao walizini huko Misri; walizini wakati wa ujana wao; huko vifua vyao vililemewa, na huko waliyabana matiti ya ubikira wao.

4Na majina yao, mkubwa aliitwa Ohola, na umbu lake Oholiba; wakawa wangu, wakazaa wana na binti. Na katika hayo majina yao, Samaria ni Ohola, na Yerusalemu ni Oholiba.

5Na Ohola alifanya mambo ya kikahaba alipokuwa wangu; naye alipenda mno wapenzi wake, Waashuri, jirani zake,

6waliovikwa samawi, maliwali na mawaziri, wote vijana wa kutamanika, wapanda farasi wakipanda farasi zao.

7Akawagawia mambo yake ya kikahaba, watu wateule wa Ashuru, wote pia; akajitia unajisi kwa vinyago vyote vya kila mmoja wa hao aliowapenda.

8Wala hakuyaacha mambo yake ya kikahaba tangu siku za Misri, kwa maana wakati wa ujana wake walilala naye, wakayabana matiti ya ubikira wake wakamwaga uzinzi wao juu yake.

9Kwa sababu hiyo nalimtia katika mikono ya wapenzi wake, katika mikono ya Waashuri, aliowapendelea.

10Na hawa wakaufunua uchi wake, wakatwaa wanawe na binti zake, wakamwua yeye kwa upanga; akawa jina la aibu kati ya wanawake; kwa maana walitoa hukumu juu yake.

11Na umbu lake, Oholiba, akayaona hayo walakini alizidi kuharibika kuliko yeye, kwa kupendelea kwake, na kwa uzinzi wake, uliokuwa mwingi kuliko uzinzi wa umbu lake.

12Aliwapendelea Waashuri, maliwali na mawaziri, jirani zake, waliovikwa nguo za shani, wapanda farasi wakipanda farasi zao, wote pia vijana wa kutamanika.

13Nikaona ya kuwa ametiwa unajisi; wote wawili walifuata njia moja.

14Naye akaongeza uzinzi wake; kwa maana aliona watu waume, ambao sura zao zimeandikwa ukutani, sura za Wakaldayo zilizoandikwa kwa rangi nyekundu;

15waliofungiwa mikumbuu viunoni mwao, na vilemba vilivyotiwa rangi vichwani mwao; wote wakuu wa kuangaliwa, kwa mfano wa wana wa Babeli katika Ukaldayo, katika nchi ya kuzaliwa kwao.

16Na mara alipowaona aliwapendelea, akatuma wajumbe kwao hata Ukaldayo.

17Na watu wa Babeli wakamwendea katika kitanda cha mapenzi, wakamtia unajisi kwa uzinzi wao, akatiwa unajisi nao, kisha roho yake ikafarakana nao.

18Basi alifunua uzinzi wake, na kufunua uchi wake; ndipo roho yangu ikafarakana naye, kama ilivyofarakana na umbu lake.

19Lakini aliongeza uzinzi wake, akikumbuka siku za ujana wake, alipofanya mambo ya kikahaba katika nchi ya Misri.

20Akawapendelea wapenzi wao, ambao nyama ya mwili wao ni kama nyama ya mwili wa punda, nacho kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi.

21Ndivyo ulivyokumbuka uasherati wa ujana wako, yalipobanwa matiti yako na Wamisri, kwa maziwa ya ujana wako.

22Kwa sababu hiyo, Ewe Oholiba, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainua wapenzi wako juu yako, ambao roho yako imefarakana nao, nami nitawaleta juu yako pande zote;

23watu wa Babeli, na Wakaldayo wote, Pekodi na Shoa na Koa, na Waashuri wote pamoja nao; vijana wa kutamanika, wote pia, maliwali na mawaziri, wakuu, na watu wenye sifa, wote wenye kupanda farasi.

24Nao watakuja kwako na silaha zao, na magari ya vita, na magurudumu, na wingi wa mataifa; watajipanga juu yako kwa ngao, na vigao, na chapeo za shaba, pande zote; nami nitawapa uwezo wa kuhukumu, nao watakuhukumu sawasawa na hukumu zao.

25Nami nitaweka wivu wangu juu yako, nao watakutenda mambo kwa ghadhabu; watakuondolea pua yako na masikio yako; na mabaki yako wataanguka kwa, upanga; watawatwaa wanao na binti zako; na mabaki yako watateketea motoni.

26Pia watakuvua nguo zako, na kukuondolea vyombo vyako vya uzuri.

27Hivyo ndivyo nitakavyoukomesha uasherati wako, na uzinzi wako, ulioletwa toka nchi ya Misri; usije ukawainulia macho yako, na kukumbuka Misri tena.

28Maana Bwana MUNGU asema hivi, Tazama nitakutia katika mikono yao unaowachukia, katika mikono yao, ambao roho imefarakana nao;

29nao watakutenda mambo kwa chuki, watakuondolea kazi zako zote, watakuacha uchi, huna nguo na aibu ya mambo yako ya kikahaba itafunuliwa, uasherati wako na uzinzi wako.

30Utatendwa mambo hayo kwa sababu umezini na hao wasioamini, na kwa sababu umetiwa unajisi kwa vinyago vyao.

31Umekwenda katika njia ya umbu lako; basi nitatia kikombe chake katika mkono wako.

32Bwana MUNGU asema hivi; Utakinywea kikombe cha umbu lako; chenye nafasi nyingi kikubwa; utadhihakiwa na kudharauliwa; kimejaa sana.

33Utajazwa ulevi na sikitiko, kwa kikombe cha ushangao na ukiwa, kikombe cha umbu lako Samaria.

34Naam, utakinywea hata hakitabaki kitu ndani yake, utavitafuna vigae vyake, utayararua maziwa yako; maana mimi, Bwana MUNGU, nimenena neno hili.

35Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umenisahau, na kunitupa nyuma yako, basi kwa hiyo, uchukue uasherati wako na uzinzi wako.

36Tena Bwana akaniambia, Mwanadamu, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi uwahubiri machukizo yao.

37Maana wamezini, na damu imo mikononi mwao, nao wamezini na vinyago vyao; tena wana wao walionizalia wamewapitisha katika moto ili waliwe nao.

38Tena wamenitenda haya; wamepatia unajisi mahali pangu patakatifu, siku ile ile, nao wamezitangua sabato zangu.

39Kwa maana walipokuwa wamekwisha kuvichinjia vinyago vyao watoto wao, ndipo walipoingia patakatifu pangu, siku ile ile, wapatie unajisi, na tazama, wamefanya hivyo kati ya nyumba yangu.

40Tena mmewatuma watu kuwaita watokao mbali; ambao mjumbe alitumwa kwao, na tazama, wakaja; nawe ulijiosha kwa ajili yao, ulitia rangi macho yako, na kujipamba vyombo vya uzuri;

41ukaketi juu ya kitanda cha enzi, na meza imeandikwa tayari mbele yake, ambayo juu yake uliweka uvumba wangu na mafuta yangu.

42Na sauti za wingi wa watu wenye hali ya raha zilikuwa pamoja naye; na pamoja na watu wasio na adabu, waliletwa walevi toka jangwani; wakawatia vikuku mikononi, na taji nzuri juu ya vichwa vyao.

43Ndipo nikasema, Huyo aliye mkongwe atafanya uzinzi! Sasa hao watazini naye, naam, na yeye!

44Wakamwingilia kama watu wamwingiliavyo kahaba; ndivyo walivyowaingilia Ohola na Oholiba, wanawake wale waasherati.

45Basi watu wenye haki watawahukumu, kwa hukumu iwapasayo wazinzi, na kwa hukumu iwapasayo wanawake wamwagao damu; kwa sababu wao ndio wazinzi, na mikononi mwao mna damu.

46Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitaleta kusanyiko la watu juu yao, nami nitawatoa warushwe huko na huko, na kutekwa nyara.

47Na kusanyiko hilo watawapiga kwa mawe, na kuwaua kwa panga zao; watawaua wana wao na binti zao, na kuziteketeza nyumba zao kwa moto.

48Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi hii, ili wanawake wote wafundishwe, wasifanye mambo ya uasherati wenu.

49Nao watawalipa ninyi malipo ya uasherati wenu, nanyi mtachukua dhambi za vinyago vyenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.