Ezekieli - Sura ya 26

Ezekieli - Sura ya 26

1Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,

2Mwanadamu, Kwa sababu Tiro amesema juu ya Yerusalemu, Aha! Yeye amevunjika aliyekuwa lango la kabila za watu; amenigeukia; nitajazwa kwa kuwa sasa ameharibika;

3basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi kupigana nawe, kama bahari iinuavyo mawimbi yake.

4Nao wataziharibu kuta za Tiro, na kuibomoa minara yake; tena nitakwangua hata mavumbi yake yamtoke, na kumfanya kuwa jabali tupu.

5Naye atakuwa mahali pa kutandazia nyavu za wavuvi kati ya bahari; maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU; naye atakuwa mateka ya mataifa.

6Na binti zake walio katika mashamba watauawa kwa upanga; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

7Maana Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitamleta Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mfalme wa wafalme, juu ya Tiro toka kaskazini, pamoja na farasi, na magari ya vita, na wapanda farasi, na jeshi, na watu wengi.

8Atawaua binti zako kwa upanga katika mashamba; naye atafanya ngome juu yako, na kufanya maboma juu yako, na kuiinua ngao juu yako.

9Naye ataweka vyombo vyake vya kubomolea mbele za kuta zako, na kwa mashoka yake ataiangusha chini minara yako.

10Kwa sababu wingi wa farasi zake, mavumbi yao yatakufunika; kuta zako zitatetemeka kwa sababu ya mshindo wa wapanda farasi, na wa magurudumu, na wa magari ya vita, atakapoingia katika malango yako, kama watu waingiavyo katika mji uliobomolewa mahali.

11Kwa kwato za farasi zake atazikanyaga njia zako zote; atawaua watu wako kwa upanga, na minara ya nguvu zako itashuka hata nchi.

12Nao wataufanya utajiri wako kuwa mateka, na bidhaa yako kuwa mawindo; nao watazibomoa kuta zako, na kuziharibu nyumba zako zipendezazo; nao wataweka mawe yako, na miti yako, na mavumbi yako, kati ya maji.

13Nami nitaikomesha sauti ya nyimbo zako, wala sauti ya vinubi vyako haitasikiwa tena.

14Nami nitakufanya kuwa jabali tupu; utakuwa mahali pa kutandazia nyavu za wavuvi; hutajengwa tena; maana mimi, Bwana, nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU.

15Bwana MUNGU amwambia Tiro neno hili; Je! Visiwa havitatikisika kwa mshindo wa kuanguka kwako, watakapougua waliojeruhiwa, yatakapofanyika machinjo kati yako.

16Ndipo wakuu wote wa bahari watashuka kutoka viti vyao vya enzi, na kuweka upande mavazi yao, na kuvua nguo zao zilizotiwa taraza; watajivika matetemeko; wataketi na kutetemeka kila dakika, na kukustaajabia,

17Nao watakufanyia maombolezo, na kukuambia, Imekuwaje wewe kuharibika, wewe uliyekaliwa na wana-maji, mji wenye sifa, uliyekuwa na nguvu katika bahari, mji huo, na hao waliokaa ndani yake, waliowatia hofu wote waliokaa ndani yake!

18Sasa visiwa vitatetemeka katika siku ya kuanguka kwako; naam, visiwa vilivyo katika bahari vitafadhaika, kwa sababu ya kuondoka kwako.

19Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitakapokufanya kuwa mji wa ukiwa, kama miji isiyokaliwa na watu; nitakapoleta vilindi vya bahari juu yako, na maji makuu yatakapokufunika;

20ndipo nitakapokushusha pamoja nao washukao shimoni, uende kwa watu wa kale; nami nitakukalisha pande za chini za nchi; mahali palipokuwa ukiwa tangu zamani, pamoja nao washukao shimoni; ili usikaliwe na watu, wala usiweke utukufu wako katika nchi yao walio hai.

21Nitakufanya kuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwako tena; ujapotafutwa, lakini hutaonekana tena kabisa, asema Bwana MUNGU.