Ezekieli - Sura ya 29

Ezekieli - Sura ya 29

1Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,

2Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao, mfalme wa Misri, ukatabiri juu yake, na juu ya Misri yote;

3nena, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa aoteaye kati ya mito yake, aliyesema, Mto wangu ni wangu mwenyewe, nami nimeufanya kwa ajili ya nafsi yangu.

4Nami nitatia kulabu katika taya zako, nami nitawashikamanisha samaki wa mito yako na magamba yako; nami nitakutoa katika mito yako, pamoja na samaki wa mito yako walioshikamana na magamba yako.

5Nami nitakuacha hali umetupwa jangwani, wewe na samaki wote wa mito yako; utaanguka juu ya uso wa uwanda; hutakusanywa, wala kuwekwa pamoja; nimekutoa uwe chakula cha wanyama wa nchi, na cha ndege wa angani.

6Na watu wote wakaao Misri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, kwa sababu wamekuwa mwanzi wa kutegemewa kwa nyumba ya Israeli.

7Walipokushika kwa mkono wako, ulivunjika, ukawararua mabega yao yote; nao walipokutegemea, ulivunjika, ukawatetemesha viuno vyao vyote.

8Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitaleta upanga juu yako, nami nitakatilia mbali nawe wanadamu na wanyama.

9Nayo nchi ya Misri itakuwa ukiwa na jangwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; kwa sababu amesema, Mto huu ni wangu, nami nimeufanya.

10Basi, tazama, mimi ni juu yako, na juu ya mito yako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa tupu, na ukiwa, toka Migdoli hata Sewene, hata mpaka wa Kushi.

11Hautapita kati yake mguu wa mwanadamu, wala hautapita kati yake mguu wa mnyama, wala haitakaliwa na watu, muda wa miaka arobaini.

12Nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake, kati ya miji iliyoharibika, itakuwa maganjo muda wa miaka arobaini; nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, nami nitawatapanya kati ya nchi mbalimbali.

13Maana Bwana MUNGU asema hivi; Mwisho wa miaka arobaini nitawakusanya Wamisri, na kuwatoa katika hizo kabila za watu, ambazo walitawanyika kati yao;

14nami nitawarejeza Wamisri walio katika hali ya kufungwa, nami nitawarudisha hata nchi ya Pathrosi, hata nchi ya kuzaliwa kwao; na huko watakuwa ufalme duni.

15Utakuwa duni kuliko falme zote; wala hautajiinua tena juu ya mataifa; nami nitawapunguza, ili wasitawale tena juu ya mataifa.

16Wala hautakuwa tena tumaini la nyumba ya Israeli, kufanya maovu yakumbukwe, watakapogeuka kuangalia nyuma yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.

17Ikawa katika mwaka wa ishirini na saba, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,

18Mwanadamu, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alilihudumisha jeshi lake huduma kuu juu ya Tiro; kila kichwa kilitiwa upaa, na kila bega liliambuliwa ngozi, lakini alikuwa hana mshahara uliotoka Tiro, wala yeye wala jeshi lake, kwa huduma ile aliyohudumu juu yake.

19Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitampa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, hiyo nchi ya Misri; naye atawachukua watu wake jamii yote pia, na kutwaa mateka yake, na kutwaa mawindo yake, nayo yatakuwa ndio mshahara wa jeshi lake.

20Nimempa nchi ya Misri kuwa malipo ya huduma aliyohudumu, kwa sababu walifanya kazi kwa ajili yangu; asema Bwana MUNGU.

21Siku ile nitawachipushia nyumba ya Israeli pembe, nami nitakujalia kufumbua kinywa kati yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.