Ezekieli - Sura ya 30

Ezekieli - Sura ya 30

1Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

2Mwanadamu, tabiri, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Pigeni makelele ya uchungu, Ole wa siku ile!

3Kwa maana siku ile i karibu, siku ile ya Bwana i karibu, siku ya mawingu; itakuwa wakati wa mataifa.

4Na upanga utakuja juu ya Misri, na dhiki itakuwa katika Kushi, watakapoanguka watu waliouawa katika Misri, nao watauondoa wingi wa watu wake, na misingi yake itabomolewa.

5Kushi, na Putu, na Ludi, na watu wote waliochanganyika, na Kubu, na wana wa nchi ya agano, wataanguka kwa upanga pamoja nao.

6Bwana asema hivi; Nao pia wanaoitegemeza Misri wataanguka, na kiburi cha uwezo wake kitashuka; toka Migdoli hata Sewene, wataanguka ndani yake kwa upanga, asema Bwana MUNGU.

7Nao watakuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake itakuwamo kati ya miji iliyoharibika.

8Nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoweka moto katika Misri, na hao wote wamsaidiao watakapoangamia.

9Katika siku hiyo watatoka wajumbe mbele zangu katika merikebu, ili kuwatia hofu Wakushi, wanaojiona kuwa salama, na dhiki itakuwa juu yao, vile vile kama katika siku ya Misri; kwa maana, tazama, inakuja.

10Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaukomesha wingi wa watu wa Misri, kwa mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli.

11Yeye, na watu wake pamoja naye, watu wa mataifa watishao, wataletwa waingie katika nchi waiharibu, nao watafuta panga zao wapigane na Misri, na kuijaza nchi wale waliouawa.

12Nami nitaikausha mito, na kuiuza nchi, na kuitia katika mikono ya watu wabaya; nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa, na watu wote walio ndani yake, kwa mkono wa wageni; mimi, Bwana, nimenena neno hili.

13Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaviharibu vinyago, nami nitavikomesha vitu vya ubatili katika Nofu, wala hapatakuwa na mkuu tena atokaye katika nchi ya Misri, nami nitatia hofu katika nchi ya Misri.

14Nami nitaifanya Pathrosi kuwa ukiwa, nami nitatia moto katika Soani, nami nitatekeleza hukumu katika No.

15Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu ya Sini, ngome ya Misri, nami nitakatilia mbali wingi wa watu wa No.

16Nami nitatia moto katika Misri; Sini itakuwa katika dhiki kuu, na No itavunjika kabisa; na Nofu itakuwa na adui wakati wa mchana.

17Vijana wa Oni, na wa Pi-besethi, wataanguka kwa upanga; na miji hiyo itakwenda utumwani.

18Huko Tapanesi nako mchana utakuwa giza, nitakapovunja huko kongwa za Misri, na kiburi cha uwezo wake kitakoma ndani yake, na katika habari zake, wingu litaifunika, na binti zake watakwenda utumwani.

19Hivyo ndivyo nitakavyotekeleza hukumu katika Misri; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

20Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa kwanza, siku ya saba ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,

21Mwanadamu, nimeuvunja mkono wa Farao, mfalme wa Misri, na tazama, haukufungwa ili kuutia dawa, haukuzongwa kwa kitambaa, upate kuwa na nguvu za kushika upanga.

22Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya Farao, mfalme wa Misri, nami nitamvunja mikono yake, mkono ulio wenye nguvu, na huo uliovunjika, nami nitauangusha upanga ulio katika mkono wake.

23Nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, na kuwatapanya kati ya nchi mbalimbali.

24Nami nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli, na kuutia upanga wangu katika mkono wake, bali mikono ya Farao nitaivunja, naye ataugua mbele yake, kwa mauguzi ya mtu aliyetiwa jeraha ya kumfisha.

25Nami nitaitegemeza mikono ya mfalme wa Babeli, na mikono ya Farao itaanguka; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoutia upanga wangu katika mkono wa mfalme wa Babeli, naye ataunyosha juu ya nchi ya Misri.

26Nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, na kuwatapanya kati ya nchi mbalimbali; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.