Ezekieli - Sura ya 32

Ezekieli - Sura ya 32

1Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,

2Mwanadamu, mfanyie Farao, mfalme wa Misri, maombolezo, umwambie, Ulifananishwa na mwana-simba wa mataifa; lakini umekuwa kama joka katika bahari; nawe watoka kwa nguvu pamoja na mito yako, na kuyachafua maji kwa miguu yako, na kuitia uchafu mito yao.

3Bwana MUNGU asema hivi; Nitautanda wavu wangu juu yako, kwa kusanyiko la watu wa kabila nyingi; nao watakuvua katika jarife langu.

4Nami nitakuacha juu ya nchi kavu, nitakutupa juu ya uso wa uwanda, nami nitawaleta ndege wote wa angani watue juu yako, nami nitawashibisha wanyama wa dunia yote kwako wewe.

5Nami nitaweka nyama yako juu ya milima, na kuyajaza mabonde kwa urefu wako.

6Tena kwa damu yako nitainywesha nchi, ambayo waogelea juu yake, hata milimani; na mifereji ya maji itajawa nawe.

7Nami nitakapokuzimisha, nitazifunikiza mbingu, na kuzifanya nyota zake kuwa giza; nami nitalifunika jua kwa wingu, wala mwezi hautatoa nuru yake.

8Mianga yote ya mbinguni iangazayo nitaifanya kuwa giza juu yako, nami nitatia giza katika nchi yako, asema Bwana MUNGU.

9Tena nitawakasirisha watu wengi mioyo yao, nitakapoleta uangamivu wako kati ya mataifa, uingie katika nchi ambazo hukuzijua.

10Nami nitawashangaza watu wa kabila nyingi kwa habari zako, na wafalme wao wataogopa sana kwa ajili yako, nitakapoutikisa upanga wangu mbele yao; nao watatetemeka kila dakika, kila mtu kwa ajili ya uhai wake, katika siku ya kuanguka kwako.

11Maana Bwana MUNGU asema hivi; Upanga wa mfalme wa Babeli utakujilia.

12Kwa panga za mashujaa nitawaangusha watu wako wote jamii; hao wote ni watu wa mataifa watishao, nao watakiharibu kiburi cha Misri, na jamii ya watu wake wengi wataangamia.

13Tena nitawaharibu wanyama wake wote, toka kando ya maji mengi; na mguu wa mwanadamu hautayatibua tena, wala kwato za mnyama hazitayatibua.

14Ndipo nitakapoyafanya maji yao kuwa safi, na kuiendesha mito yao kama mafuta, asema Bwana MUNGU.

15Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa na jangwa, nchi iliyopungukiwa na vitu vilivyoijaza, nitakapowapiga watu wote wakaao ndani yake, ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

16Hayo ndiyo maombolezo watakayoomboleza; binti za mataifa wataomboleza kwa hayo; kwa hayo wataomboleza kwa ajili ya Misri, na kwa ajili ya watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.

17Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la Bwana likanijia kusema,

18Mwanadamu, walilie watu wa Misri. Wote jamii ukawabwage, naam, yeye, na binti za mataifa mashuhuri, hata pande za chini za nchi, pamoja na watu washukao shimoni.

19Umemshinda nani kwa uzuri? Shuka, ukalazwe pamoja na wasiotahiriwa.

20Wataanguka kati ya watu waliouawa kwa upanga; ametokwa apigwe na upanga; mvuteni aende mbali pamoja na watu wake wote jamii.

21Walio hodari watasema naye, toka kati ya kuzimu pamoja nao wamsaidiao; wameshuka wamelala kimya, hata wasiotahiriwa, hali wameuawa kwa upanga.

22Ashuru yuko huko, na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga,

23ambao makaburi yao yamewekwa pande za shimo zilizo mbali sana, wote jamii wamezunguka kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, waliofanya utisho katika nchi yao walio hai.

24Elamu yuko huko, na watu wake wote jamii, pande zote za kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, walioshuka hali hawana tohara hata pande za chini ya nchi; ambao waliwatia watu hofu katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni.

25Wamemwekea kitanda kati ya hao waliouawa, pamoja na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana maogofyo yao yalifanyika katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni; amewekwa kati ya hao waliouawa.

26Mesheki yuko huko, na Tubali, na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana walifanya utisho wao katika nchi ya walio hai.

27Je! Wasilale pamoja na mashujaa wao wasiotahiriwa, walioanguka, walioshuka kuzimu pamoja na silaha zao za vita, ambao wameweka panga zao chini ya vichwa vyao, na maovu yao mifupani mwao? Maana waliwatisha mashujaa katika nchi ya walio hai.

28Lakini utavunjika kati ya hao wasiotahiriwa, nawe utalala pamoja nao waliouawa kwa upanga.

29Edomu yuko huko, wafalme wake, na wakuu wake wote, ambao katika uwezo wao wamelazwa pamoja nao waliouawa kwa upanga; watalala pamoja na hao wasiotahiriwa, na pamoja na hao washukao shimoni.

30Wakuu wa kaskazini wako huko, wote pia, na Wasidoni, wote walioshuka pamoja na hao waliouawa; kwa sababu ya utisho walioufanya katika uwezo wao wamefedheheka, nao wamelala hali hawana tohara, pamoja nao waliouawa kwa upanga, nao wanachukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni.

31Farao atawaona, naye atapata faraja juu ya watu wake wote jamii; naam, Farao, jeshi lake lote waliouawa kwa upanga, asema Bwana MUNGU.

32Kwa maana nimeweka utisho wake katika nchi ya walio hai; naye atalazwa kati yao wasiotahiriwa, pamoja na hao waliouawa kwa upanga; yeye Farao na watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.