Ezekieli - Sura ya 33

Ezekieli - Sura ya 33

1Neno la Bwana likanijia, kusema,

2Mwanadamu, sema na wana wa watu wako, uwaambie, Hapo nitakapoleta upanga juu ya nchi, watu wa nchi hiyo wakimtwaa mtu mmoja miongoni mwao, na kumweka awe mlinzi wao;

3ikiwa, aonapo upanga unakuja juu ya nchi hiyo, apiga tarumbeta na kuwaonya watu;

4basi mtu awaye yote aisikiaye sauti ya tarumbeta, wala haonywi, upanga ukija na kumwondoa, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.

5Aliisikia sauti ya tarumbeta, wala hakuonywa; damu yake itakuwa juu yake; lakini kama angalionywa, angalijiokoa roho yake.

6Bali mlinzi akiona upanga unakuja, kama hapigi tarumbeta, wala watu hawakuonywa, na upanga ukaja ukamwondoa mtu awaye yote miongoni mwao; ameondolewa huyo katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwa mlinzi huyo.

7Basi wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu.

8Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.

9Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako.

10Na wewe, mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli; Ninyi mwasema hivi, kwamba, Makosa yetu na dhambi zetu ni juu yetu, nasi tumedhoofika katika dhambi hizo; basi tungewezaje kuwa hai?

11Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?

12Na wewe, mwanadamu, waambie wana wa watu wako, Haki yake mwenye haki haitamwokoa, katika siku ya kukosa kwake; na kwa habari ya uovu wake mtu mwovu, hataanguka kwa ajili ya uovu huo, siku ile atakapoghairi na kuuacha uovu wake; wala yeye aliye mwenye haki hataweza kuishi kwa haki yake, siku ile atakapotenda dhambi.

13Nimwambiapo mwenye haki, ya kwamba hakika ataishi; kama akiitumainia haki yake, akatenda uovu, basi katika matendo yake ya haki, hata mojawapo halitakumbukwa; bali katika uovu wake alioutenda, atakufa katika uovu huo.

14Tena, nimwambiapo mtu mwovu, Hakika utakufa; kama akighairi, na kuiacha dhambi yake, na kutenda yaliyo halali na haki;

15kama mtu mwovu akirudisha rehani, na kumrudishia mtu mali yake aliyomnyang'anya, akizifuata sheria za uzima, asitende uovu wo wote; hakika ataishi, hatakufa.

16Katika dhambi zake zote alizozitenda, hata mojawapo haitakumbukwa juu yake; ametenda yaliyo halali na haki; hakika ataishi.

17Walakini wana wa watu wako husema, Njia ya Bwana si sawa; lakini watu hao, njia yao si sawa.

18Mwenye haki ageukapo, na kuiacha haki yake, na kutenda maovu, atakufa katika maovu hayo.

19Na mtu mbaya ageukapo, na kuuacha ubaya wake, na kutenda yaliyo halali na haki, ataishi kwa matendo hayo.

20Lakini ninyi husema, Njia ya Bwana si sawa. Ee nyumba ya Israeli, nitawahukumu ninyi; kila mtu kwa kadiri ya njia zake.

21Ikawa, katika mwaka wa kumi na mbili wa kuhamishwa kwetu, mwezi wa kumi, siku ya tano ya mwezi, mtu mmoja aliyekuwa ametoroka toka Yerusalemu akanijia, akisema, Mji umepigwa.

22Basi mkono wa Bwana umekuwa juu yangu wakati wa jioni, kabla hajafika yeye aliyetoroka; naye alikuwa amenifumbua kinywa changu, hata aliponijia wakati wa asubuhi; na kinywa changu kilikuwa wazi, wala sikuwa bubu tena.

23Neno la Bwana likanijia, kusema,

24Mwanadamu, watu wale wakaao mahali palipoharibika katika nchi ya Israeli husema ya kwamba, Ibrahimu alikuwa mmoja, akairithi nchi hii; lakini sisi tu watu wengi; tumepewa nchi hii iwe urithi wetu.

25Basi, waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Mnakula nyama pamoja na damu yake, na kuviinulia vinyago vyenu macho yenu, na kumwaga damu; je, mtaimiliki nchi hii?

26Mnategemea upanga wenu, mnatenda machukizo, mnanajisi kila mtu mke wa jirani yake; je! Mtaimiliki nchi hii?

27Hivi ndivyo utakavyowaambia, Bwana MUNGU asema hivi; Kama mimi niishivyo, hakika watu wale wakaao mahali palipoharibika wataanguka kwa upanga, naye mtu aliye katika uwanda, nitamtoa na kuwapa wanyama wakali, ili aliwe; na hao walio ndani ya ngome na mapango watakufa kwa tauni.

28Nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, na kiburi cha uwezo wake kitakoma; nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa, asipite mtu.

29Ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, kwa sababu ya machukizo yao yote waliyoyatenda.

30Nawe, mwanadamu, wana wa watu wako husimulia habari zako karibu na kuta, na ndani ya milango ya nyumba zao, na kuambiana, kila mtu na ndugu yake, wakisema, Haya! Twende tukasikie ni neno gani hilo litokalo kwa Bwana.

31Nao huja kwako kama watu wajavyo, nao hukaa mbele yako kama watu wangu, nao husikia maneno yako, wasiyatende; maana kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye upendo mwingi, lakini mioyo yao inatafuta faida yao.

32Na tazama, wewe umekuwa kwao kama wimbo mzuri sana, wa mtu mwenye sauti ipendezayo, awezaye kupiga kinanda vizuri; maana, wasikia maneno yako, lakini hawayatendi.

33Na hayo yatakapokuwapo (tazama, yanakuja), ndipo watakapojua ya kuwa nabii amekuwapo kati yao.