Ezekieli - Sura ya 36

Ezekieli - Sura ya 36

1Na wewe, mwanadamu, itabirie milima ya Israeli, useme, Enyi milima ya Israeli, lisikieni neno la Bwana.

2Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu adui amesema juu yenu, Aha! Na, Mahali pa juu pa zamani pamekuwa petu tupamiliki;

3basi tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu, naam, kwa sababu wamewafanya ninyi kuwa ukiwa, na kuwameza pande zote, mpate kuwa milki kwa mabaki ya mataifa, nanyi mmeambwa kwa midomo yao waongeao, na kwa masingizio ya watu;

4kwa sababu hiyo, enyi milima ya Israeli, lisikieni neno la Bwana MUNGU; Bwana MUNGU aiambia hivi hiyo milima na vilima, mifereji ya maji na mabonde, mahali palipoharibika na kuwa ukiwa, na miji iliyoachwa na watu, ambayo imekuwa mateka, na kuzomewa na mabaki ya mataifa, walio karibu pande zote;

5basi Bwana MUNGU asema hivi; Hakika kwa moto wa wivu wangu nimenena juu ya mabaki ya mataifa, na juu ya Edomu yote, waliojiandikia nchi yangu kuwa milki yao, kwa furaha ya mioyo yao yote, kwa jeuri ya roho zao, ili waitupe nje kuwa mawindo;

6basi katika kutabiri habari za nchi ya Israeli, uiambie milima na vilima, mifereji ya maji na mabonde, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nimenena katika wivu wangu na hasira yangu, kwa sababu mmechukua aibu ya mataifa;

7basi Bwana MUNGU asema hivi; Nimeinua mkono wangu, kusema, Hakika, mataifa walio karibu nanyi pande zote, wao watachukua aibu yao.

8Lakini ninyi, enyi milima ya Israeli, mtachipuza matawi yenu na kuwapa watu wangu Israeli matunda yenu; maana wa karibu kuja.

9Maana, tazama, mimi nasimama upande wenu, nami nitawaelekea, nanyi mtalimwa na kupandwa mbegu;

10nami nitaongeza watu juu yenu, nyumba yote ya Israeli, naam, yote pia; nayo miji itakaliwa na watu, na mahali palipoharibika patajengwa.

11Nami nitaongeza juu yenu mwanadamu na mnyama, nao watazidi na kuzaa; nami nitawakalisha watu ndani yenu, kwa kadiri ya hali yenu ya kwanza, nami nitawatendea mema kuliko mema ya mianzo yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

12Naam, nitaleta watu watembee juu yenu, naam, watu wangu Israeli; nao watakumiliki, nawe utakuwa urithi wao, wala hutawafisha watoto wao tena tangu leo.

13Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa watu hukuambia, wewe nchi u mwenye kula watu, nawe umekuwa mwenye kufisha watu wa taifa lako;

14basi hutakula watu tena, wala hutafisha watu wa taifa lako tena, asema Bwana MUNGU;

15wala sitakusikizisha tena aibu yao wasioamini, wala hutachukua matukano ya watu tena; wala hutalikwaza taifa lako tena, asema Bwana MUNGU.

16Tena, neno la Bwana likanijia, kusema,

17Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokaa katika nchi yao wenyewe, waliitia uchafu kwa njia yao na kwa matendo yao. Njia yao mbele zangu ilikuwa kama uchafu wa mwanamke wakati wa kutengwa kwake.

18Kwa hiyo nalimwaga hasira yangu juu yao, kwa ajili ya damu waliyoimwaga juu ya nchi, na kwa sababu wameitia uchafu kwa vinyago vyao.

19Nikawatawanya katika mataifa, wakatapanyika katika nchi nyingi; kwa kadiri ya njia yao, na kwa kadiri ya matendo yao, naliwahukumu.

20Nao walipoyafikilia mataifa yale waliyoyaendea, walilitia unajisi jina langu takatifu; kwa kuwa watu waliwanena, wakisema, Watu hawa ni watu wa Bwana, nao wametoka katika nchi yake.

21Lakini, naliwahurumia kwa ajili ya jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli walikuwa wamelitia unajisi katika mataifa waliyoyaendea.

22Kwa hiyo; waambieni nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi Sitendi hili kwa ajili yenu, Ee nyumba ya Israeli, bali kwa ajili ya jina langu takatifu, mlilolitia unajisi katika mataifa mliyoyaendea.

23Nami nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, asema Bwana MUNGU, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao.

24Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe.

25Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote.

26Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.

27Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.

28Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

29Nami nitawaokoeni na uchafu wenu wote; nitaiita ngano, na kuiongeza, wala sitaweka njaa juu yenu tena.

30Nami nitazidisha matunda ya miti, na mazao ya mashamba, msipate tena kutukanwa na mataifa kwa sababu ya njaa.

31Ndipo mtazikumbuka njia zenu mbaya, na matendo yenu yasiyokuwa mema, nanyi mtajichukia nafsi zenu kwa macho yenu, kwa sababu ya maovu yenu na machukizo yenu.

32Ijulikane kwenu ya kuwa silitendi neno hili kwa ajili yenu, asema Bwana MUNGU; tahayarikeni, na kufadhaika, kwa sababu ya njia zenu, Enyi nyumba ya Israeli.

33Bwana MUNGU asema hivi; Siku ile nitakapowatakaseni na maovu yenu yote, nitaifanya miji ikaliwe na watu, na palipobomolewa pajengwe tena.

34Nchi iliyokuwa ukiwa italimwa, ijapokuwa ilikuwa ukiwa mbele ya macho ya watu wote waliopita.

35Nao watasema, Nchi hii, iliyokuwa ukiwa, imekuwa kama bustani ya Adeni; nayo miji iliyokuwa mahame, na ukiwa, na magofu, sasa ina maboma, inakaliwa na watu.

36Ndipo mataifa, waliobaki karibu yenu pande zote, watajua ya kuwa mimi, Bwana, nimejenga mahali palipoharibika, nami nimepanda mbegu katika nchi iliyokuwa ukiwa; mimi, Bwana, nimesema hayo; tena nitayatenda.

37Bwana MUNGU asema hivi, Tena kwa ajili ya jambo hili nitaulizwa na nyumba ya Israeli, ili niwatendee; nami nitawaongeza kwa watu kama kundi la kondoo.

38Kama kundi lililo tayari kutolewa sadaka, kama kundi la Yerusalemu katika sikukuu zake zilizoamriwa; ndivyo itakavyojazwa watu, miji ile iliyokuwa maganjo; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.