Ezekieli - Sura ya 43

Ezekieli - Sura ya 43

1Kisha akanileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki;

2na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling'aa kwa utukufu wake.

3Na maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona nilipokuja kuuharibu mji; nayo maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona karibu na mto wa Kebari; nikaanguka kifudifudi.

4Na huo utukufu wa Bwana ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki.

5Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana uliijaza nyumba.

6Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami.

7Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele; na nyumba ya Israeli hawatalinajisi jina langu takatifu tena, wao, wala wafalme wao, kwa mambo yao ya kikahaba, na kwa mizoga ya wafalme wao, katika mahali pao pa juu;

8kwa kuweka kizingiti chao karibu na kizingiti changu; na mwimo wao karibu na mwimo wangu; tena palikuwa na ukuta tu kati ya mimi na wao; nao wamelinajisi jina langu takatifu kwa machukizo yao waliyoyatenda; basi, kwa sababu hiyo, nimewakomesha katika hasira yangu.

9Basi sasa wayaondoe mambo yao ya kikahaba, na mizoga ya wafalme wao, yawe mbali nami, nami nitakaa kati yao milele.

10Na wewe, mwanadamu, waonyeshe wana wa Israeli nyumba hii, ili wayatahayarikie maovu yao; na waipime hesabu yake.

11Na ikiwa wameyatahayarikia yote waliyoyatenda, waonyeshe umbo la nyumba, na namna yake, na matokeo yake, na maingilio yake, na maumbo yake yote, na maagizo yake yote, na kawaida zake zote, na sheria zake zote, ukayaandike machoni pao; ili walishike umbo lake lote, na maagizo yake, na kuyatenda.

12Hii ndiyo sheria ya nyumba; juu ya kilele cha mlima, mpaka wake wote pande zote patakuwa patakatifu sana. Tazama, hii ndiyo sheria ya nyumba.

13Na vipimo vya madhabahu kwa dhiraa ni hivi; (dhiraa ni dhiraa na shubiri); tako lake ni dhiraa moja, na upana wake dhiraa moja; na pambizo yake karibu na ncha yake pande zote, shubiri moja; na hili litakuwa tako la madhabahu.

14Tena toka chini, juu ya nchi, hata daraja ya chini, dhiraa mbili, na upana wake dhiraa moja; tena toka daraja ndogo hata daraja kubwa, dhiraa nne, na upana wake dhiraa moja.

15Na madhabahu ya juu itakuwa dhiraa nne; na toka madhabahu pawashwapo moto na kwenda juu zitakuwa pembe nne.

16Na pale pawashwapo moto, urefu wake dhiraa kumi na mbili, na upana wake kumi na mbili, mraba pande zake nne.

17Na daraja, urefu wake dhiraa kumi na nne, na upana wake dhiraa kumi na nne, pande zake nne; na pambizo yake nusu dhiraa; na tako lake dhiraa moja, kote kote, na madaraja yake yataelekea upande wa mashariki.

18Kisha akaniambia, Mwanadamu, Bwana MUNGU asema hivi; Hizi ndizo sheria za madhabahu katika siku ile watakapoifanya, ili watoe sadaka za kuteketezwa juu yake, na kunyunyiza damu juu yake.

19Utawapa makuhani Walawi, walio wa uzao wa Sadoki, walio karibu nami, ili kunihudumu, asema Bwana MUNGU, ng'ombe mume mchanga awe sadaka ya dhambi.

20Nawe utatwaa baadhi ya damu yake, na kuitia juu ya pembe zake nne, na juu ya ncha nne za daraja, na juu ya pambizo yake pande zote; ndivyo utakavyoitakasa, na kuifanyia upatanisho.

21Tena utamtwaa ng'ombe wa sadaka ya dhambi, naye utamteketeza mahali palipoamriwa pa nyumba ile, nje ya mahali patakatifu.

22Na siku ya pili utamtoa beberu mkamilifu awe sadaka ya dhambi; nao wataisafisha madhabahu, kama walivyoisafisha kwa ng'ombe huyo.

23Utakapokwisha kuitakasa, utatoa ng'ombe mume mchanga mkamilifu, na kondoo mume wa kundini mkamilifu.

24Nawe utawaleta karibu mbele za Bwana, na makuhani watamwaga chumvi juu yao, nao watawatoa wawe sadaka za kuteketezwa kwa Bwana.

25Kwa muda wa siku saba utaweka tayari mbuzi kila siku awe sadaka ya dhambi; pia wataweka tayari ng'ombe mume mchanga, na kondoo mume wa kundini, wakamilifu.

26Kwa muda wa siku saba wataifanyia madhabahu upatanisho, na kuitakasa; ndivyo watakavyoiweka wakfu.

27Nao watakapozitimiza siku hizo, itakuwa, siku ya nane na baadaye, makuhani watatoa sadaka zenu za kuteketezwa juu ya madhabahu, na sadaka zenu za amani nami nitawakubali ninyi, asema Bwana MUNGU.