Ezekieli - Sura ya 47

Ezekieli - Sura ya 47

1Baadaye akanileta tena mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu.

2Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume.

3Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, kwenda masharikini, akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpaka viweko vya miguu.

4Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno.

5Kisha akapima dhiraa elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika.

6Akaniambia, Mwanadamu, je! Umeona haya? Kisha akanichukua akanirudisha mpaka ukingo wa mto.

7Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana, upande huu na upande huu.

8Ndipo akaniambia, Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari

9Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo.

10Tena itakuwa, wavuvi watasimama karibu nao; toka Engedi mpaka En-eglaimu, patakuwa ni mahali pa kutandazia nyavu; samaki wao watakuwa namna zao mbalimbali, kama samaki wa bahari kubwa, wengi sana.

11Bali mahali penye matope, na maziwa yake, hayataponywa; yataachwa yawe ya chumvi.

12Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.

13Bwana MUNGU asema hivi; Huu ndio mpaka ambao mtaigawanya nchi iwe urithi sawasawa na kabila kumi na mbili za Israeli; kwa Yusufu, mafungu mawili.

14Nanyi mtaimiliki, mtu huyu sawasawa na huyu; ambayo naliuinua mkono wangu kuwapa baba zenu; na nchi hii itawaangukia kuwa urithi.

15Na huu ndio mpaka wa nchi; upande wa kaskazini, toka bahari kubwa, kwa njia ya Hethloni, mpaka maingilio ya Sedada;

16Hamathi, na Berotha, na Sibraimu, ulio katikati ya mpaka wa Dameski na mpaka wa Hamathi; na Haser-hatikoni, ulio karibu na mpaka wa Haurani.

17Nao mpaka toka baharini utakuwa Hasar-enoni, penye mpaka wa Dameski, na kaskazini kuelekea upande wa kaskazini ndio mpaka wa Hamathi. Huu ndio upande wa kaskazini.

18Na upande wa mashariki, kati ya Haurani na Dameski, na Gileadi na nchi ya Israeli, utakuwa mto Yordani; mtapima toka mpaka wa upande wa kaskazini hata bahari ya mashariki. Huu ndio upande wa mashariki.

19Na upande wa kusini, kuelekea kusini, utakuwa ni kutoka Tamari mpaka maji ya Meriba-Kadeshi, mpaka kijito cha Misri, mpaka bahari kubwa. Huu ndio upande wa kusini, kuelekea kusini.

20Na upande wa magharibi, utakuwa ni bahari kubwa, kutoka mpaka wa kusini mpaka mahali penye kuelekea maingilio ya Hamathi. Huu ndio upande wa magharibi.

21Basi ndivyo mtakavyojigawanyia nafsi zenu nchi hii, sawasawa na kabila za Israeli.

22Tena itakuwa mtaigawanya kwa kura, kuwa urithi kwenu, na kwa wageni wakaao kwenu hali ya ugeni, watakaozaa watoto kati yenu, nao watakuwa kwenu, kama wazaliwa miongoni mwa wana Israeli; watakuwa na urithi pamoja nanyi kati ya kabila za Israeli.

23Tena itakuwa, mgeni akaaye katika kabila iwayo yote, atapewa urithi katika kabila asema Bwana MUNGU.