Ezra - Sura ya 7

1Ikawa baada ya mambo hayo, wakati wa kutawala kwake Artashasta, mfalme wa Uajemi, Ezra, mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia,
2mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu,
3mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi,
4mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki,
5mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, kuhani mkuu;
6huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa, aliyokuwa ameitoa Bwana, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa Bwana, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye.
7Nao wakakwea baadhi ya wana wa Israeli, na wa makuhani, na wa Walawi, na waimbaji, na mabawabu, na Wanethini, ili kwenda Yerusalemu, katika mwaka wa saba wa mfalme Artashasta.
8Naye Ezra akafika Yerusalemu mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa huyo mfalme.
9Maana alianza kukwea kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akafika Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kama mkono mwema wa Mungu wake ulivyokuwa pamoja naye.
10Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli.
11Basi hii ndiyo nakala ya waraka, mfalme Artashasta aliyompa Ezra, kuhani, mwandishi, naam, mwandishi wa maneno ya amri za Bwana, na wa sheria zake alizowapa Israeli.
12Artashasta, mfalme wa wafalme, kwa Ezra, kuhani, mwandishi wa torati ya Mungu wa mbinguni, salamu kamili; wakadhalika.
13Natoa amri ya kwamba wote walio wa watu wa Israeli, na makuhani wao, na Walawi, katika ufalme wangu, wenye nia ya kwenda Yerusalemu kwa hiari yao wenyewe, waende pamoja nawe.
14Kwa kuwa umetumwa na mfalme, na washauri wake saba, ili kuuliza habari za Yuda na Yerusalemu, kwa sheria ya Mungu wako iliyo mkononi mwako;
15na kuichukua fedha na dhahabu, ambayo mfalme, na washauri wake, kwa hiari yao, wamemtolea Mungu wa Israeli, akaaye Yerusalemu;
16na fedha yote na dhahabu utakayoona katika wilaya ya Babeli, pamoja na vitu watakavyotoa watu kwa hiari yao, na vitu vya makuhani walivyotoa kwa hiari yao, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu.
17Kwa sababu hiyo ujitahidi kununua kwa fedha hiyo mafahali, kondoo waume, wana-kondoo, pamoja na sadaka zao za unga, na sadaka zao za kinywaji; nawe utazitoa juu ya madhabahu ya nyumba ya Mungu wenu, iliyoko Yerusalemu.
18Na neno lo lote mtakaloona vema kulitenda, wewe na ndugu zako, kwa ile fedha na dhahabu itakayobaki, hilo litendeni, kama apendavyo Mungu wenu.
19Na vile vyombo upewavyo kwa huduma ya nyumba ya Mungu wako, virejeze mbele za Mungu wa Yerusalemu.
20Na cho chote kitakachohitajiwa zaidi, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wako, kitakachokupasa kukitoa, kitoe katika nyumba ya hazina ya mfalme.
21Na mimi, naam mimi, mfalme Artashasta, nawapa amri wote wenye kutunza hazina, walio ng'ambo ya Mto, ya kwamba, kila neno ambalo Ezra, kuhani, mwandishi wa torati ya Mungu wa mbinguni, atalitaka kwenu, na litendeke kwa bidii nyingi,
22hata kiasi cha talanta mia za fedha, na vipimo mia vya ngano, na bathi mia za divai, na bathi mia za mafuta, na chumvi bila kuuliza kiasi chake.
23Kila neno litakaloamriwa na Mungu wa mbinguni, na litendeke halisi kwa ajili ya nyumba ya Mungu wa mbinguni. Kwa nini itokee ghadhabu juu ya ufalme wa mfalme na wanawe?
24Tena twawaarifuni ya kuwa katika habari ya makuhani, na Walawi, na waimbaji, na mabawabu na Wanethini, au watumishi wa nyumba hii ya Mungu, si halali kuwatoza kodi, wala ada, wala ushuru.
25Na wewe, Ezra, kwa kadiri ya hekima ya Mungu wako iliyo mkononi mwako, waweke waamuzi na makadhi, watakaowahukumu watu wote walio ng'ambo ya Mto, yaani, wote wenye kuzijua amri za Mungu wako; ukamfundishe yeye asiyezijua.
26Na kila mtu asiyekubali kuitenda sheria ya Mungu wako, na sheria ya mfalme, na apatilizwe hukumu kwa bidii, kwamba ni kuuawa, au kwamba ni kuhamishwa, au kuondolewa mali yake, au kufungwa.
27Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa baba zetu, aliyetia neno kama hilo katika moyo wa mfalme, kuipamba nyumba ya Bwana iliyoko Yerusalemu.
28Naye amenifikilizia rehema zake mbele ya mfalme, na washauri wake, na mbele ya wakuu wote wa mfalme wenye mamlaka. Nami nikatiwa nguvu, kwa kadiri mkono wa Bwana, Mungu wangu, ulivyokuwa pamoja nami, nikawakusanya wakuu wote katika Israeli, ili wakwee pamoja nami.