Ezra - Sura ya 8

Ezra - Sura ya 8

1Basi hawa ndio wakuu wa mbari za baba zao, na hii ndiyo nasaba ya wale waliokwea pamoja nami kutoka Babeli, wakati wa kutawala kwake mfalme Artashasta.

2Wa wana wa Finehasi, Gershoni; wa wana wa Ithamari, Danieli; wa wana wa Daudi, Hatushi, mwana wa Shekania;

3wa wana wa Paroshi, Zekaria; na pamoja naye wakahesabiwa kwa nasaba wanaume mia na hamsini.

4Wa wana wa Pahath-Moabu, Eliehoenai, mwana wa Zerahia; na pamoja naye wanaume mia mbili;

5Wa wana wa Zatu, Shekania, mwana wa Yahazieli; na pamoja naye wanaume mia tatu.

6Na wa wana wa Adini, Ebedi, mwana wa Yonathani; na pamoja naye wanaume hamsini.

7Na wa wana wa Elamu, Yeshaya, mwana wa Athalia; na pamoja naye wanaume sabini.

8Na wa wana wa Shefatia, Zebadia, mwana wa Mikaeli; na pamoja naye wanaume themanini.

9Wa wana wa Yoabu, Obadia, mwana wa Yehieli; na pamoja naye wanaume mia mbili na kumi na wanane.

10Na wa wana wa Binui, Shelomithi, mwana wa Yosifia; na pamoja naye wanaume mia na sitini.

11Na wa wana wa Bebai, Zekaria, mwana wa Bebai; na pamoja naye wanaume ishirini na wanane.

12Na wa wana wa Azgadi, Yohana, mwana wa Hakatani; na pamoja naye wanaume mia na kumi.

13Na wa wana wa Adonikamu, hawa waliokuwa wa mwisho, na hayo ndiyo majina yao, Elifeleti, na Yeueli, na Shemaya; na pamoja nao wanaume sitini.

14Na wa wana wa Bigwai, Uthai, mwana wa Zabudi; na pamoja naye wanaume sabini.

15Nikawakusanya penye mto ushukao kwenda Ahava; na huko tukapiga kambi yetu muda wa siku tatu; nikawakagua watu, na makuhani, wala sikuona hapo wana wa Lawi hata mmoja.

16Ndipo nikatuma watu kwenda kumwita Eliezeri, na Arieli, na Shemaya, na Elnathani, na Yaribu, na Elnathani, na Nathani, na Zekaria, na Meshulamu, waliokuwa wakuu; na Yoyaribu, na Elnathani pia, waliokuwa waalimu.

17Nikawapeleka kwa Ido, mkuu, huko Kasifia; nikawaambia watakayomwambia Ido, na ndugu zake hao Wanethini, huko Kasifia, kwamba watuletee watu watakaohudumu katika nyumba ya Mungu wetu.

18Na kama mkono mwema wa Mungu wetu ulivyokuwa pamoja nasi, wakamletea Ishekeli,

19na Hashabia, na pamoja naye Yeshaya, wa wana wa Merari, na ndugu zake na wana wao, watu ishirini;

20na katika Wanethini, ambao Daudi, na wakuu, walikuwa wamewaweka kwa ajili ya utumishi wa Walawi, Wanethini mia mbili na ishirini; wote wametajwa kwa majina yao.

21Ndipo nikaamuru kufunga, hapo penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za Mungu, na kutafuta kwake njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe, na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote.

22Maana naliona haya kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapanda farasi, ili kutusaidia juu ya adui njiani; kwa maana tulikuwa tumesema na mfalme, tukinena, Mkono wa Mungu u juu ya watu wote wamtafutao, kuwatendea mema; bali uweza wake na ghadhabu yake ni kinyume cha wote wamwachao.

23Basi tukafunga, tukamsihi Mungu wetu kwa ajili ya hayo; naye akatutakabali.

24Ndipo nikawatenga watu kumi na wawili wa wakuu wa makuhani, nao ni Sherebia, na Hashabia, na watu kumi wa ndugu zao pamoja nao,

25nami nikawapimia kwa mizani zile fedha, na dhahabu, na vile vyombo, matoleo kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu, ambayo mfalme, na washauri wake, na wakuu wake, na Israeli wote waliokuwapo, walikuwa wameyatoa;

26nami nikawapimia mikononi mwao talanta za fedha mia sita na hamsini na vyombo vya fedha talanta mia; na talanta mia za dhahabu;

27na mabakuli ishirini ya dhahabu, thamani yake darkoni elfu; na vyombo viwili vya shaba nzuri iliyong'aa, thamani yake sawa na dhahabu.

28Kisha nikawaambia, Ninyi mmekuwa watakatifu kwa Bwana, na hivyo vyombo ni vitakatifu; na fedha na dhahabu ni matoleo ya hiari kwa Bwana, Mungu wa baba zenu.

29Basi, angalieni, na kuvitunza vitu hivi, hata mtakapovipima mbele ya wakuu wa makuhani, na Walawi, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli, huko Yerusalemu, katika vyumba vya nyumba ya Bwana.

30Hivyo makuhani na Walawi wakaupokea uzani wa fedha, na dhahabu, na vyombo, ili kuvileta Yerusalemu nyumbani kwa Mungu wetu.

31Ndipo tukasafiri toka mtoni Ahava siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza, ili kwenda Yerusalemu; na mkono wa Mungu ulikuwa pamoja nasi, akatuokoa na mkono wa adui, na mtu mwenye kutuvizia njiani.

32Tukafika Yerusalemu, tukakaa huko muda wa siku tatu.

33Hata siku ya nne, hizo fedha na dhahabu na vile vyombo vilipimwa ndani ya nyumba ya Mungu, vikatiwa mikononi mwa Meremothi, mwana wa Uria, kuhani; na pamoja naye alikuwapo Eleazari, mwana wa Finehasi; na pamoja nao Yozabadi, mwana wa Yeshua, na Noadia, mwana wa Binui, Walawi;

34vile vyombo vyote kwa hesabu na kwa uzani; tena uzani wake wote uliandikwa wakati ule.

35Na wana wa uhamisho, waliokuwa wametoka katika uhamisho wakamtolea Mungu wa Israeli sadaka za kuteketezwa, ng'ombe kumi na wawili kwa ajili ya Israeli wote, na kondoo waume tisini na sita, na wana-kondoo sabini na saba, na mbuzi waume kumi na wawili, kuwa sadaka ya dhambi, hao wote pia walikuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana.

36Wakawapa manaibu wa mfalme, na maliwali wa ng'ambo ya Mto, maagizo ya mfalme; nao wakawapa watu, na nyumba ya Mungu, msaada.