Mwanzo - Sura ya 12

Mwanzo - Sura ya 12

1Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;

2nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;

3nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.

4Basi Abramu akaenda, kama Bwana alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.

5Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani.

6Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo.

7Bwana akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea.

8Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea Bwana madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana.

9Naye Abramu akasafiri, akazidi kwenda pande za kusini.

10Basi kulikuwa njaa katika nchi ile; Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa nzito katika nchi.

11Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso;

12basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai.

13Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako.

14Basi ikawa Abramu alipofika Misri, Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana.

15Wakuu wa Farao wakamwona, nao wakamsifu kwa Farao; basi yule mwanamke akachukuliwa nyumbani mwa Farao.

16Naye akamtendea Abramu mema kwa ajili yake; naye alikuwa na kondoo na ng'ombe, na punda waume, na watumwa, na wajakazi, na punda wake, na ngamia.

17Lakini Bwana akampiga Farao na nyumba yake mapigo makuu, kwa ajili ya Sarai, mkewe Abramu.

18Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, N'nini hili ulilonitendea? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo?

19Mbona ulisema, Huyo ni umbu langu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako.

20Farao akawaagiza watu kwa ajili yake, wakampeleka njiani, na mkewe, na kila alichokuwa nacho.