Mwanzo - Sura ya 13

Mwanzo - Sura ya 13

1Abramu akapanda kutoka Misri, yeye, na mkewe, na kila alichokuwa nacho, na Lutu pamoja naye, mpaka kusini.

2Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu.

3Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza kati ya Betheli na Ai;

4napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la Bwana hapo.

5Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng'ombe na kondoo, na hema.

6Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja.

7Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi.

8Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu.

9Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto.

10Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla Bwana hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya Bwana, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari.

11Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao.

12Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma.

13Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya Bwana.

14Bwana akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi;

15maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele.

16Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi; hata mtu akiweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, uzao wako nao utahesabika.

17Ondoka, ukatembee katika nchi hii katika mapana yake, na marefu yake, maana nitakupa wewe nchi hiyo.

18Basi Abramu akajongeza hema yake, akaja akakaa kwenye mialoni ya Mamre, nayo ni miti iliyoko Hebroni, akamjengea Bwana madhabahu huko.