Mwanzo - Sura ya 14

Mwanzo - Sura ya 14

1Ikawa siku za Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme wa Elamu na Tidali mfalme wa Goimu,

2walifanya vita na Bera mfalme wa Sodoma na Birsha mfalme wa Gomora, na Shinabu mfalme wa Adma, na Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari.

3Hawa wote wakakutana panapo bonde la Sidimu, kwenye Bahari ya Chumvi.

4Miaka kumi na miwili walimtumikia Kedorlaoma, hata mwaka wa kumi na tatu wakaasi.

5Na mwaka wa kumi na nne akaja Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja naye, wakawapiga Warefai katika Ashteroth-karnaimu, na Wazuzi katika Hamu, na Waemi katika Shawe-kiryathaimu,

6na Wahori katika mlima wao Seiri, mpaka Elparani iliyo karibu na jangwa.

7Kisha wakarudi wakaja mpaka Enmisfati, ndio Kadeshi, wakapiga nchi yote ya Waamaleki, na Waamori waliokaa Hasason-tamari.

8Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa Adma, na mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka wakapanga vita panapo bonde la Sidimu;

9wapigane na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, wafalme wanne juu ya wale watano.

10Na bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora wakakimbia, wakaanguka huko, nao waliosalia wakakimbia milimani.

11Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao.

12Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao.

13Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda, akampasha habari Abramu Mwebrania; naye amekaa panapo mialoni ya Mamre, yule Mwamori, ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na Abramu.

14Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani.

15Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski.

16Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.

17Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme.

18Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana.

19Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi.

20Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.

21Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe.

22Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa Bwana, Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi,

23ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu ya kiatu wala cho chote kilicho chako, usije ukasema, Nimemtajirisha Abramu;

24isipokuwa hivyo walivyokula vijana, na sehemu za watu waliokwenda nami, yaani, Aneri, na Eshkoli, na Mamre; na watwae wao sehemu zao.