Mwanzo - Sura ya 21
1Bwana akamjia Sara kama alivyonena, na Bwana akamfanyia kama alivyosema.
2Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu.
3Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia.
4Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru.
5Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka.
6Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami.
7Akasema, N'nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake.
8Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya.
9Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka.
10Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.
11Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe.
12Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.
13Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako.
14Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba.
15Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja.
16Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia.
17Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko.
18Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa.
19Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana.
20Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.
21Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.
22Ikawa wakati ule Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakamwambia Ibrahimu, wakinena, Mungu yu pamoja nawe katika yote unayotenda.
23Basi sasa uniapie kwa Mungu, ya kuwa hutanitenda hila, wala mwanangu, wala mjukuu wangu, lakini kwa kadiri ya fadhili niliyokutendea utanitendea mimi, na nchi hii ambayo umetembea ndani yake.
24Ibrahimu akasema, Nitaapa.
25Kisha Ibrahimu akamlaumu Abimeleki kwa sababu ya kisima cha maji ambacho watumwa wa Abimeleki wamekinyang'anya.
26Abimeleki akasema, Mimi sijui ni nani aliyetenda neno hili, wala hukuniambia, wala sikusikia habari hii ila leo tu.
27Ibrahimu akatwaa kondoo na ng'ombe akampa Abimeleki, na hao wawili wakafanya mapatano.
28Ibrahimu akaweka wana kondoo wa kike saba peke yao.
29Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Hawa wana kondoo wa kike saba, uliowaweka peke yao, maana yake nini?
30Akasema, Hawa wana kondoo wa kike saba utawapokea mkononi mwangu, wawe ushuhuda ya kuwa ni mimi niliyekichimba kisima hiki.
31Kwa hiyo akapaita mahali pale Beer-sheba, kwa sababu waliapa huko wote wawili.
32Basi wakafanya mapatano huko Beer-sheba. Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakaondoka wakarudi hata nchi ya Wafilisti.
33Ibrahimu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaliitia huko jina la Bwana Mungu wa milele.
34Ibrahimu akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Wafilisti siku nyingi.

Swahili
Italiano (it-IT)
Português do Brasil (pt-BR)
Polski (PL)
Deutsch (Deutschland)
Français (France)
Español (España)
Українська Біблія у перекладі Огієнка
English Bible - 21ST CENTURY KING JAMES (KJ21)