Mwanzo - Sura ya 22

Mwanzo - Sura ya 22

1Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.

2Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.

3Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu.

4Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali.

5Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena.

6Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja.

7Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa?

8Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja.

9Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni.

10Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.

11Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.

12Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee.

13Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.

14Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire,

15Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni

16akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,

17katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;

18na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.

19Basi Ibrahimu akawarudia vijana wake, wakaondoka, wakaenda zao pamoja mpaka Beer-sheba; Ibrahimu akakaa huko Beer-sheba.

20Ikawa baada ya mambo hayo, Ibrahimu akaambiwa ya kwamba, Tazama, Milka naye amemzalia Nahori ndugu yako wana;

21Usi, mzaliwa wa kwanza wake, na Buzi nduguye, na Kemueli, baba wa Aramu;

22na Kesedi, na Hazo, na Pildashi, na Yidlafu, na Bethueli.

23Bethueli akamzaa Rebeka; hao wanane Milka alimzalia Nahori ndugu wa Ibrahimu.

24Na suria wake Reuma naye alizaa Teba na Gahamu na Tahashi na Maaka.