Mwanzo - Sura ya 23

Mwanzo - Sura ya 23

1Basi umri wake Sara ulikuwa miaka mia na ishirini na saba ndio umri wake Sara.

2Sara akafa katika Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu akaja kumlilia Sara na kumwombolezea.

3Akaondoka Ibrahimu kutoka mbele ya maiti wake, akasema na wazawa wa Hethi, akinena,

4Mimi ni mgeni, ninatembea kwenu; nipeni mahali pa kuzikia kwenu, pawe pangu, nimzike maiti wangu atoke mbele yangu.

5Wazawa wa Hethi wakamjibu Ibrahimu, wakamwambia,

6Utusikie, Ee bwana, ndiwe mtu mkuu sana kwetu, uzike maiti wako katika kaburi lile utakalochagua katika makaburi yetu. Hapana mtu kwetu atakayekuzuilia kaburi lake, usizike maiti wako.

7Ibrahimu akaondoka, akainama mbele ya watu wa nchi, mbele ya hao wazawa wa Hethi.

8Naye akazungumza nao, akisema, Ikiwa nia yenu nimzike maiti wangu atoke mbele yangu, mnisikie, mkaniombee kwa Efroni bin Sohari,

9ili kwamba anipe pango ya Makpela, iliyo katika mpaka wa shamba lake, na anipe kwa kima kilicho kamili, katikati yenu, iwe milki yangu ya kuzikia.

10Basi Efroni alikuwa akiketi kati ya wazawa wa Hethi. Efroni Mhiti akamjibu Ibrahimu, na wazawa wa Hethi wanasikiliza, hata watu wote waingiao mlango wa mji wake, akisema,

11Sivyo, bwana wangu, unisikilize. Lile shamba nakupa, na pango iliyomo nakupa; mbele ya wana wa watu wangu nakupa, uzike maiti wako.

12Ibrahimu akainama mbele ya watu wa nchi.

13Akamwambia Efroni, na watu wa nchi wanasikiliza, akisema, Tafadhali unisikilize; nitatoa kima cha shamba, nawe ukipokee kwangu, nami nitamzika humo maiti wangu.

14Efroni akamjibu Ibrahimu, akamwambia,

15Bwana wangu, unisikilize. Sehemu ya nchi, ambayo thamani yake ni shekeli za fedha mia nne, n'nini hii baina yako na yangu? Basi uzike maiti wako.

16Ibrahimu akakubali maneno ya Efroni. Ibrahimu akampimia Efroni ile fedha aliyotaja masikioni mwa wazawa wa Hethi, shekeli za fedha mia nne za namna inayotumika na wenye biashara.

17Basi shamba la Efroni lililokuwa katika Makpela kuelekea Mamre, shamba, na pango iliyokuwamo, na miti yote iliyokuwamo shambani, iliyokuwa katika mipaka yake pande zote, vyote viliyakinishwa

18kuwa mali yake Ibrahimu, mbele ya wazawa wa Hethi, mbele ya watu wote waingiao katika mlango wa mji wake.

19Basi baada ya hayo Ibrahimu akamzika Sara mkewe katika pango ya shamba la Makpela kuelekea Mamre, ndiyo Hebroni, katika nchi ya Kanaani.

20Na lile shamba, na pango iliyomo, iliyakinishwa kuwa mali yake Ibrahimu na wazawa wa Hethi, kuwa mahali pa kuzikia.