Mwanzo - Sura ya 26

1Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari.
2Bwana akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia.
3Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako.
4Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia.
5Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu.
6Isaka akakaa katika Gerari.
7Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso.
8Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe.
9Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni ndugu yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nalisema, Nisife kwa ajili yake.
10Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani.
11Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa.
12Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, Bwana akambariki.
13Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana.
14Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu.
15Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi.
16Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi.
17Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko.
18Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye.
19Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika.
20Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye.
21Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna.
22Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa Bwana ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.
23Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba.
24Bwana akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu.
25Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko.
26Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake.
27Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu?
28Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba Bwana alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe
29ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa Bwana.
30Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa.
31Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaapiana wao kwa wao, kisha Isaka akawapa ruhusa, nao wakaenda zao kwa amani.
32Ikawa siku ileile, watumwa wa Isaka wakaja wakampasha habari za kile kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, Tumeona maji.
33Naye akakiita jina lake Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba, hata leo.
34Esau alipokuwa mwenye miaka arobaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti.
35Roho zao Isaka na Rebeka zikajaa uchungu kwa ajili yao.