Mwanzo - Sura ya 29

1Kisha Yakobo akashika njia yake, akafika nchi ya wana wa mashariki.
2Naye akaangalia, na tazama, kiko kisima kondeni, na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu nacho, kwa sababu katika kisima kile hunywesha makundi; na palikuwa na jiwe kubwa juu ya kinywa cha kisima.
3Makundi yote hukusanyika huko, watu wakafingirisha hilo jiwe katika kinywa cha kisima wakawanywesha kondoo, na kulirudisha jiwe juu ya kinywa cha kisima mahali pake.
4Yakobo akawauliza, Ndugu zangu, watu wa wapi ninyi? Wakasema, Tu wa Harani sisi.
5Akawauliza, Je! Mnamjua Labani, mwana wa Nahori? Wakasema, Tunamjua.
6Akawauliza, Je! Hajambo? Wakasema, Hajambo; tazama, Raheli binti yake anakuja na kondoo.
7Akasema, Tazama, ukali mchana bado, wala sio wakati wa kukusanya wanyama; wanywesheni kondoo, mwende kuwalisha.
8Wakasema, Hatuwezi, hata yakusanyike makundi yote, watu wakafingirishe jiwe katika kinywa cha kisima, ndipo tunapowanywesha kondoo.
9Hata alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo za baba yake, maana aliwachunga.
10Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo za Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulifingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo za Labani, ndugu wa mamaye.
11Yakobo akambusu Raheli, akainua sauti yake akalia.
12Yakobo akamwarifu Raheli ya kuwa yeye ni ndugu wa babaye, na ya kuwa ni mwana wa Rebeka. Basi akapiga mbio akampasha babaye habari.
13Ikawa Labani aliposikia habari za Yakobo, mwana wa nduguye, akaenda mbio amlaki, akamkumbatia, akambusu, akamleta nyumbani kwake. Naye akamwambia Labani maneno hayo yote.
14Labani akamwambia, Ndiwe kweli mfupa wangu na nyama yangu. Naye akakaa kwake muda wa mwezi mmoja.
15Labani akamwambia Yakobo, Kwa sababu wewe ni ndugu yangu, basi, je! Unitumikie bure? Niambie mshahara wako utakuwa nini?
16Labani alikuwa na binti wawili, jina la mkubwa ni Lea, na jina la mdogo ni Raheli.
17Naye Lea macho yake yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso.
18Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo.
19Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa kwangu.
20Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda.
21Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu, maana siku zangu zimetimia; niingie kwake.
22Labani akakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya karamu.
23Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake, akamletea Yakobo, naye akaingia kwake.
24Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa, awe mjakazi wake.
25Ikawa, kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani, Nini hii uliyonitenda?
26Sikukutumikia kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani akasema, Havitendeki hivi kwetu, kumtoa mdogo kabla ya mkubwa;
27timiza siku zake saba, nasi tutakupa huyu naye kwa utumishi utakaonitumikia, miaka saba mingine.
28Yakobo akafanya hivi, akatimiza siku zake saba. Naye akampa Raheli binti yake kuwa mkewe.
29Labani akampa binti yake Raheli mjakazi wake Bilha, awe mjakazi wake.
30Akaingia kwa Raheli naye, akampenda Raheli kuliko Lea, akatumika kwa ajili yake miaka saba mingine.
31Bwana akaona ya kwamba Lea hakupendwa, naye akafungua tumbo lake; bali Raheli alikuwa hazai.
32Lea akapata mimba akazaa mwana, akampa jina lake, Reubeni, maana alisema, Kwa kuwa Bwana ameona teso langu; sasa mume wangu atanipenda.
33Akapata mimba tena akazaa mwana, akasema, Kwa kuwa Bwana amesikia ya kwamba mimi sikupendwa, amenipa na huyu; akamwita jina lake Simeoni.
34Akapata mimba tena, akazaa mwana, akasema, Basi wakati huu mume wangu ataungana nami, kwa sababu nimemzalia wana watatu. Kwa hiyo akamwita jina lake Lawi.
35Akapata mimba tena, akazaa mwana. Akasema, Mara hii nitamsifu Bwana; kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; akaacha kuzaa.