Mwanzo - Sura ya 35

Mwanzo - Sura ya 35

1Mungu akamwambia Yakobo, Ondoka, panda uende Betheli, ukakae huko; ukamfanyie Mungu madhabahu huko; yeye aliyekutokea ulipomkimbia Esau, ndugu yako.

2Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu.

3Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea.

4Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na pete zilizokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu.

5Wakashika njia, hofu ya Mungu ikaishika miji iliyowazunguka, wala hawakuwafuata wana wa Yakobo.

6Basi Yakobo akafika Luzu, ulio katika nchi ya Kanaani, ndio Betheli, yeye na watu wote waliokuwa pamoja naye.

7Akajenga huko madhabahu, akapaita mahali pale, El-Betheli; kwa sababu huko Mungu alimtokea, hapo alipomkimbia ndugu yake.

8Akafa Debora mlezi wa Rebeka, akazikwa chini ya Betheli, chini ya mwaloni; na jina lake likaitwa Alon-bakuthi.

9Mungu akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki.

10Mungu akamwambia, Jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli.

11Mungu akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uzidi ukaongezeke. Taifa na kundi la mataifa watatoka kwako, na wafalme watatoka viunoni mwako.

12Na nchi hii niliyowapa Ibrahimu na Isaka nitakupa wewe, na uzao wako baada yako nitawapa nchi hiyo.

13Mungu akakwea juu kutoka kwake mahali hapo aliposema naye.

14Yakobo akasimamisha nguzo mahali aliposema naye, nguzo ya mawe, akamimina juu yake sadaka ya kinywaji, akamimina mafuta juu yake.

15Yakobo akapaita mahali pale, Mungu aliposema naye, Betheli.

16Wakasafiri kutoka Betheli, hata ukabaki mwendo wa kitambo tu kufika Efrathi, Raheli akashikwa na utungu wa kuzaa, na utungu wake ulikuwa mzito.

17Ikawa alipokuwa anashikwa sana na utungu, mzalisha akamwambia, Usiogope, maana sasa utamzaa mwanamume mwingine.

18Ikawa hapo katika kutoa roho yake, maana alikufa, akamwita jina lake Benoni, lakini babaye alimwita Benyamini.

19Akafa Raheli, akazikwa katika njia ya Efrathi, ndio Bethlehemu.

20Yakobo akasimamisha nguzo juu ya kaburi lake, ndiyo nguzo ya kaburi la Raheli hata leo.

21Kisha akasafiri Israeli akapiga hema yake upande wa pili wa mnara wa Ederi.

22Ikawa Israeli alipokuwa akikaa katika nchi ile, Reubeni akaenda akalala na Bilha, suria wa babaye; Israeli akasikia habari. Basi hao wana wa Yakobo walikuwa kumi na wawili.

23Wana wa Lea ni Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, na Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Zabuloni.

24Wana wa Raheli, ni Yusufu na Benyamini.

25Wana wa Bilha, kijakazi wa Raheli, ni Dani na Naftali.

26Wana wa Zilpa, kijakazi wa Lea, ni Gadi na Asheri. Hawa ndio wana wa Yakobo aliozaliwa katika Padan-aramu.

27Yakobo akaja kwa Isaka, babaye, huko Mamre, mji wa Arba, ndio Hebroni, walipokaa ugenini Ibrahimu na Isaka.

28Siku za Isaka zilikuwa miaka mia na themanini.

29Naye Isaka akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake, ni mzee, ameshiba siku. Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika