Mwanzo - Sura ya 39

Mwanzo - Sura ya 39

1Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri naye Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli waliomleta huko.

2Bwana akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri.

3Bwana wake akaona ya kwamba Bwana yu pamoja naye, na ya kuwa Bwana anafanikisha mambo yote mkononi mwake.

4Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake.

5Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, Bwana akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba.

6Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu.

7Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami.

8Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu.

9Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?

10Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye.

11Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani;

12huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje.

13Ikawa alipoona ya kwamba amemwachilia nguo yake mkononi mwake, naye amekimbia nje,

14akawaita watu wa nyumbani mwake, akasema nao, akinena, Angalieni, ametuletea mtu Mwebrania atufanyie dhihaka. Ameingia kwangu, ili alale nami, nikalia kwa sauti kuu.

15Ikawa, aliposikia ya kuwa nimepaza sauti yangu na kulia, aliiacha nguo yake kwangu, akakimbia, akatoka nje.

16Basi akaiweka ile nguo kwake hata bwana wake aje nyumbani.

17Naye akamwambia kama maneno hayo, akisema, Yule mtumwa Mwebrania uliyemleta kwetu, aliingia kwangu anidhihaki.

18Ikawa nilipopaza sauti yangu, nikalia, akaacha nguo yake kwangu akakimbia nje.

19Ikawa bwana wake aliposikia maneno ya mkewe aliyomwambia, akisema, Mtumwa wako amenitendea mambo kama haya, hasira yake ikawaka.

20Bwana wake akamtwaa Yusufu, akamtia gerezani, mahali walipofungwa wafungwa wa mfalme, naye akawamo humo gerezani.

21Lakini Bwana akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza.

22Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya.

23Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu; kwa kuwa Bwana alikuwa pamoja naye. Bwana akayafanikisha yote aliyoyafanya.