Mwanzo - Sura ya 4

Mwanzo - Sura ya 4

1Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana.

2Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.

3Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana.

4Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake;

5bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.

6Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?

7Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.

8Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani].

9Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?

10Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.

11Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;

12utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani.

13Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.

14Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.

15Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga.

16Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni.

17Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko; akajenga mji akauita Henoko, kwa jina la mwanawe.

18Henoko akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; Methushaeli akamzaa Lameki.

19Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila.

20Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama.

21Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi.

22Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama.

23Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua;

24Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba.

25Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.

26Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana.