Mwanzo - Sura ya 40

Mwanzo - Sura ya 40

1Ikawa, baada ya mambo hayo, mnyweshaji wa mfalme wa Misri, na mwokaji wake, wakamkosa bwana wao, mfalme wa Misri.

2Farao akawaghadhibikia maakida wake wawili, mkuu wa wanyweshaji na mkuu wa waokaji.

3Akawatia katika lindo nyumbani mwa mkuu wa askari, humo gerezani, mahali alipofungwa Yusufu.

4Mkuu wa askari akamwekea Yusufu watu hao, naye akawahudumu, nao wakakaa siku kadha wa kadha katika kifungo.

5Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani.

6Yusufu akawajia asubuhi, akawaona wamefadhaika.

7Akawauliza hao maakida wa Farao, waliokuwa pamoja naye katika kifungo, nyumbani mwa bwana wake, akisema, Mbona nyuso zenu zimekunjamana leo?

8Wakamwambia, Tumeota ndoto wala hapana awezaye kuifasiri. Yusufu akawaambia, Kufasiri si kazi ya Mungu? Tafadhalini mniambie.

9Mnyweshaji mkuu akamhadithia Yusufu ndoto yake; akamwambia, Katika ndoto yangu nimeota, uko mzabibu mbele yangu.

10Na katika mzabibu mlikuwa na matawi matatu, nao ulikuwa kana unamea, unachanua maua, vishada vyake vikatoa zabibu zilizoiva.

11Na kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, nikampa Farao kikombe mkononi mwake.

12Yusufu akamwambia, Tafsiri yake ndiyo hii. Matawi matatu ni siku tatu.

13Baada ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako, atakurudisha katika kazi yako; nawe utampa Farao kikombe mkononi mwake, kama desturi ya kwanza, ulipokuwa mnyweshaji wake.

14Ila unikumbuke mimi, utakapopata mema, ukanifanyie fadhili, nakuomba, ukanitaje kwa Farao, na kunitoa katika nyumba hii.

15Kwa sababu hakika naliibiwa kutoka nchi ya Waebrania, wala hapa sikutenda neno lo lote hata wanitie gerezani.

16Mkuu wa waokaji alipoona ya kwamba hiyo tafsiri ni ya mema, akamwambia Yusufu, Mimi kadhalika nilikuwa katika ndoto yangu, na tazama, ziko nyungo tatu za mikate myeupe juu ya kichwa changu.

17Na katika ungo wa juu, mlikuwa na kila namna ya chakula kwa Farao, kazi za mwokaji; ndege wakavila katika ungo juu ya kichwa changu.

18Yusufu akajibu, akasema, Tafsiri yake ndiyo hii Nyungo tatu ni siku tatu.

19Baada ya siku tatu Farao atakiinua na kukuondolea kichwa chako, na kukutundika juu ya mti, na ndege watakula nyama yako.

20Ikawa siku ya tatu, siku ya kuzaliwa kwake Farao, akawafanyia karamu watumwa wake wote; akakiinua kichwa cha mkuu wa wanyweshaji, na cha mkuu wa waokaji, miongoni mwa watumwa wake.

21Akamrudisha mkuu wa wanyweshaji katika kazi yake ya kunywesha, naye akampa Farao kikombe mkononi mwake.

22Bali akamtundika mkuu wa waokaji, kama Yusufu alivyowafasiria.

23Lakini huyo mkuu wa wanyweshaji hakumkumbuka Yusufu, alimsahau.