Mwanzo - Sura ya 46

Mwanzo - Sura ya 46

1Akasafiri Israeli, pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye.

2Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa.

3Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko.

4Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako.

5Yakobo akaondoka kutoka Beer-sheba; wana wa Israeli wakamchukua baba yao na watoto wao wadogo, na wake zao katika magari aliyoyapeleka Farao ili kumchukua.

6Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamezipata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye.

7Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri.

8Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli walioingia Misri, Yakobo na wanawe: Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.

9Na wana wa Reubeni; Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi.

10Na wana wa Simeoni; Yemueli na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli, mwana wa mwanamke Mkanaani.

11Na wana wa Lawi; Gershoni, na Kohathi, na Merari.

12Na wana wa Yuda; Eri, na Onani, na Shela, na Peresi, na Zera; lakini Eri na Onani walikufa katika nchi ya Kanaani. Na wana wa Peresi, ni Hesroni, na Hamuli.

13Na wana wa Isakari; Tola, na Puva, na Yashubu, na Shimroni.

14Na wana wa Zabuloni; Seredi, na Eloni, na Yaleeli.

15Hao ndio wana wa Lea, aliomzalia Yakobo katika Padan-aramu, na Dina, binti yake. Nafsi zote za wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu.

16Na wana wa Gadi; Sefoni, na Hagi, na Shuni, na Esboni, na Eri, na Arodi, na Areli.

17Na wana wa Asheri; Imna, na Ishva, na Ishvi, na Beria, na Sera, umbu lao. Na wana wa Beria ni Heberi, na Malkieli.

18Hao ndio wana wa Zilpa, ambaye Labani alimpa Lea, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao, nafsi kumi na sita.

19Wana wa Raheli, mkewe Yakobo Yusufu na Benyamini.

20Walizaliwa kwake Yusufu katika nchi ya Misri, Manase na Efraimu, aliomzalia Asenathi binti Potifera, kuhani wa Oni.

21Na wana wa Benyamini; Bela, na Bekeri, na Ashbeli, na Gera, na Naamani, na Ehi, na Roshi, na Mupimu, na Hupimu, na Ardi.

22Hao ndio wana wa Raheli, aliomzalia Yakobo, nafsi zote walikuwa kumi na wanne.

23Na wana wa Dani; Hushimu.

24Na wana wa Naftali; Yaseeli, na Guni, na Yaseri, na Shilemu.

25Hao ndio wana wa Bilha, ambaye Labani alimpa Raheli, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao; nafsi zote walikuwa saba.

26Nafsi zote waliokuja pamoja na Yakobo mpaka Misri waliotoka viunoni mwake, bila wake za wanawe Yakobo, nafsi zote walikuwa sitini na sita.

27Na wana wa Yusufu aliozaliwa katika Misri walikuwa nafsi wawili. Nafsi zote za nyumba ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini.

28Yakobo akampeleka Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni.

29Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionyesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake kitambo kizima.

30Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai.

31Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, Nitapanda mimi nimpashe Farao habari; nitamwambia, Ndugu zangu, na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kanaani, wamenijia.

32Na watu hao ni wachungaji, maana wamekuwa watu wa kuchunga wanyama, nao wameleta kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo.

33Itakuwa Farao atakapowaita, na kuwauliza, Kazi yenu ni nini?

34Semeni, Watumwa wako tumekuwa wachunga wanyama tangu ujana wetu, na hata leo, sisi, na baba zetu; mpate kukaa katika nchi ya Gosheni; maana kila mchunga wanyama ni chukizo kwa Wamisri.