Mwanzo - Sura ya 48

Mwanzo - Sura ya 48

1Ikawa, baada ya mambo hayo, Yusufu akaambiwa, Tazama, baba yako hawezi; akawatwaa wanawe wawili, Manase na Efraimu, pamoja naye.

2Naye akaarifiwa Yakobo ya kwamba, Angalia, mwanao Yusufu anakuja kwako. Israeli akajitia nguvu, akaketi juu ya kitanda.

3Yakobo akamwambia Yusufu, Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu, katika nchi ya Kanaani, akanibariki,

4akaniambia, Mimi hapa, nitakuongezea uzao wako, na kukuzidisha, nami nitakufanya uwe kundi la mataifa; kisha nitawapa wazao wako nchi hii baada yako, iwe milki ya milele.

5Basi sasa wanao wawili uliozaliwa katika nchi ya Misri kabla sijaja kwako Misri ni watoto wangu, yaani, Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama Reubeni na Simeoni.

6Na wazao wako utakaozaa baada ya hawa watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao.

7Na mimi nilipokuja kutoka Padan, Raheli akanifia katika nchi ya Kanaani, njiani, si mwendo mkubwa kabla ya kufika Efrathi. Nikamzika katika njia ya Efrathi, ndio Bethlehemu.

8Israeli akawaona wana wa Yusufu, akasema, Ni nani hawa?

9Yusufu akamwambia babaye, Hawa ni wanangu, Mungu alionipa hapa. Akasema, Tafadhali uwalete kwangu nami nitawabariki.

10Na macho ya Israeli yalikuwa mazito kwa uzee, wala hakuweza kuona. Akawaleta kwake, naye akawabusu, na kuwakumbatia.

11Israeli akamwambia Yusufu, Sikudhani ya kwamba nitakuona uso wako, na Mungu amenionyesha na uzao wako pia.

12Yusufu akawatoa katika magoti yake, naye akainama kifudifudi

13Yusufu akawaweka wote wawili, Efraimu katika mkono wake wa kuume, kuelekea mkono wa kushoto wa Israeli; na Manase katika mkono wake wa kushoto, kuelekea mkono wa kuume wa Israeli, akawasogeza karibu naye.

14Israeli akanyosha mkono wake wa kuume akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, aliyekuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, huku akijua atiavyo mikono; maana Manase ndiye aliyezaliwa kwanza.

15Akambariki Yusufu, akasema, Mungu ambaye baba zangu, Ibrahimu na Isaka, walienenda mbele zake, yeye Mungu aliyenilisha, maisha yangu yote, hata siku hii ya leo,

16naye Malaika aliyeniokoa na maovu yote, na awabariki vijana hawa; jina langu na litajwe juu yao, na jina la baba zangu, Ibrahimu na Isaka; na wawe wingi wa watu kati ya nchi.

17Yusufu alipoona kwamba babaye anaweka mkono wake wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, ikawa vibaya machoni pake. Akauinua mkono wa babaye auondoe katika kichwa cha Efraimu, ili auweke juu ya kichwa cha Manase.

18Yusufu akamwambia babaye, Sivyo, babangu, maana huyu ni mzaliwa wa kwanza; weka mkono wako wa kuume kichwani pake.

19Babaye akakataa, akasema, Najua, mwanangu najua, yeye naye atakuwa taifa, yeye naye atakuwa mkuu; lakini ndugu yake mdogo atakuwa mkubwa kuliko yeye, na uzao wake watakuwa wingi wa mataifa.

20Akawabariki siku ile akasema, Katika ninyi Waisraeli watabariki, wakisema, Mungu na akufanye kama Efraimu na Manase. Akamweka Efraimu mbele ya Manase.

21Israeli akamwambia Yusufu, Angalia, mimi ninakufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, naye atawarudisha mpaka nchi ya baba zenu.

22Nami nimekupa wewe sehemu moja zaidi kuliko ndugu zako, niliyoitwaa katika mikono ya Waamori, kwa upanga wangu na upinde wangu.