Mwanzo - Sura ya 7

1Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki.
2Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke.
3Tena katika ndege wa angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote.
4Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arobaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali.
5Nuhu akafanya kama vile Bwana alivyomwamuru.
6Naye Nuhu alikuwa mtu wa miaka mia sita hapo hiyo gharika ya maji ilipokuwa juu ya nchi.
7Nuhu akaingia katika safina, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kwa sababu ya maji ya gharika.
8Na katika wanyama walio safi, na wanyama wasio safi, na ndege, navyo vyote vitambaavyo juu ya nchi,
9wakaingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, mume na mke, kama vile Mungu alivyomwamuru Nuhu.
10Ikawa baada ya siku hizo saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi.
11Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka.
12Mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arobaini mchana na usiku.
13Siku ile ile Nuhu akaingia katika safina, yeye, na Shemu na Hamu na Yafethi, wana wa Nuhu, na mkewe Nuhu, na wake watatu wa wanawe pamoja naye;
14wao na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi, kwa jinsi yake, na kirukacho kwa jinsi yake, kila ndege wa namna yo yote.
15Waliingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, wa kila chenye mwili kilicho na pumzi ya uhai ndani yake.
16Na walioingia, waliingia mume na mke, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; Bwana akamfungia.
17Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arobaini; nayo maji yakazidi, yakaieleza safina, ikaelea juu ya nchi.
18Maji yakapata nguvu, yakazidi sana juu ya nchi; na ile safina ikaelea juu ya uso wa maji.
19Maji yakapata nguvu sana sana juu ya nchi; na milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikizwa.
20Maji yakapata nguvu, hata ikafunikwa milima kiasi cha mikono kumi na mitano.
21Wakafa wote wenye mwili waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu;
22kila kitu chenye pumzi ya roho ya uhai puani mwake kikafa, kila kilichokuwako katika nchi kavu.
23Kila kilicho hai juu ya uso wa nchi kikafutiliwa mbali tangu mwanadamu hata mnyama wa kufugwa, na kitambaacho, na ndege wa angani; vilifutiliwa mbali katika nchi, akabaki Nuhu tu, na hao walio pamoja naye katika safina.
24Maji yakapata nguvu juu ya nchi siku mia na hamsini.